Kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya jeshi la polisi Wilayani Kilombero kutotimiza wajibu wao wa kulinda raia na mali zao, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe. Hamad Masauni amewasimamisha kazi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilombero (OCD) Shedrack Kigobanya pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai wa Wilaya hiyo Daudi Mshana ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa dhidi yao.
Waziri Masauni amechukua uamuzi huo Februari 20 mwaka huu wakati wa hotuba yake mbele ya wananchi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyoko katika Mji mdogo wa Ifakara Mkoani Morogoro.
Mhe. Masauni amesema amegundua uwepo wa mapungufu mengi ambayo yamepelekea wananchi kuwa na kero nyingi dhidi ya OCD Huyo na kuwaasababishia matatizo mengi, sababu kuu ni kushindwa kusimamia vema kazi yake ya kuhakikisha kuwa jeshi la Polisi katika Wilaya hiyo inatekeleza majukumu yake ipasavyo.
“...nataka niwaambieni Serikali yenu ya awamu ya sita haitakubali kuona mwananchi yoyote anaonewa... na ndio maana tunamsimamisha kazi mara moja OCD wa hapa ameshindwa kusimamia kazi yake vizuri ya jeshi la Polisi katika Wilaya hii...."amesema Waziri Masauni.
Aidha, Mhe. Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi hapa nchini kuhakikisha kuwa linaimarisha mifumo ya utendaji kazi kuanzia ngazi ya kata hadi Mkoa, wakati huo huo Waziri huyo amewataka wananchi kuimarisha ushirikiano baina yao na Jeshi la polisi ili kufichua viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Moja ya kero kubwa zilizotajwa na wananchi ni Askari wa jeshi hilo kuwanyanyasa wananchi, kutofanyia kazi malalamiko kwa wakati pamoja na kuwanyang'anya mali wananchi hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Kassim Nakapala ameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo.
Nae, Bwana Boniface Mmanga mkazi wa Ifakara amesema Jeshi la Polisi ndiyo tegemezi katika kulinda usalama wa raia na mali zao hapa nchini lakini, polisi katika Wilaya ya Kilombero wamekuwa kero kubwa kwa wananchi hali ambayo imewafanya kukosa imani kwa jeshi hilo na kumuomba Waziri huyo wa kuwapatia ufumbuzi juu ya kero zao zinazosababishwa na jeshi la Polisi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.