PROF, SHEMDOE AWATAKA MAAFISA WA SEKTA YA MISITU, NYUKI KUIBUA SHOROBA NA KUJENGA VIWANDA VYA NYUKI
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa wa Sekta ya Mali asili na Sekta ya Nyuki hapa Nchini kuja na mipango ya kuibua shoroba za wanyama zinazohitajika na kukuza viwanda vya nyuki na kuhakikisha vinajengwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya kuinua mapato ya Halmashauri na Taifa kwa jumla.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja ndiye alikuwa mgeni Rasmi kwenye kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe
Prof. Shemdoe amesema hayo Machi 17 mwaka huu kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa wa Sekta ya Mali asili na Sekta ya Nyuki kwa niaba yake kilichofanyika katika hoteli ya Flomi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Katibu Mkuu huyo amesema, kikao hicho cha siku tatu kinachoshirikisha Maafisa wa Sekta ya Mali Asili, nyuki na Maafisa Wanyama Pori kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini kina lengo la kuimarisha Sekta hizo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Washiriki wa Kikao kazi wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Mariam Mtunguja (katikati waliokaa)
Pia mesema, kikao kina lengo la kuimarisha utendaji kazi wa Maafisa wa Sekta ya Mali Asili na nyuki kwa ajili ya kuendeleza mifumo ya Kiikolojia na Uchumi wa Taifa.
Hata hivyo Prof. Shemdoe amewataka maafisa wa Sekta ya Mali asili kuibua Shoroba nyingine na kuweka mikakati namna ya Shoruba hizo zitakavyofaidisha wananchi wanazunguka maeneo hayo huku akiwataka Maafisa nyuki kukuza na kuendeleza viwanda vya nyuki ili kukuza utalii kwenye misitu na nyuki.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi
“mnatakiwa kuibua shoroba zinazohitajika na namna shoroba hizo zitakavyoinua kipato cha mwananchi na kuondoa migogoro ya wanyama pori wakati wakiharibu mazao yao” amesema Katibu Mkuu.
“Katika Sekta ya nyuki Mpango utusaidie kukuza Sekta ya nyuki na kuendeleza viwanda vya nyuki kwa kuhakikisha uendelevu wa viwanda hivyo na vingine viweze kujengwa kwenye Halmashauri zetu.
Sekta zote hizo zikiwekwa vizuri uhifadhi katika mamlaka za Serikali za Mitaa utaimarika na tutapata mazingira rahisi ya kuendeleza sekta ya Utalii na kuona namna Sekta hiyo itakavyochangia mapato katika Serikali za Mitaa na Taifa kwa jumla” ameongeza Prof. Shemdoe.
Katika hatua nyingine Prof. Shemdoe amewapongeza Maafisa wa Sekta ya Mali Asili na Nyuki pamoja na wale wa Wanyama Pori kwa namna ambavyo kwa muda mrefu wamefanya kazi katika mazingira magumu kwa kukosa vitendea kazi kama Rasilimali Fedha, rasilimali watu na vyombo vya Usafiri na kwamba anatambua changamoto zao na anazendelea kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Misitu Tanzania kutoka Shirika la World widelife Fund (WWF) Dkt. Lawrence Mbwambo amesema lengo la Shirika hilo kuwakutanisha Maafisa wa Sekta ya Misitu na nyuki ni kutaka kutathmini kazi wanazozifanya na kwa kushirikiana na shirika hilo waweze kuweka malengo ya pamoja na shirika hilo ya kurejesha misitu iliyoko chini ya TAMISEMI pamoja na kuboresha maisha ya watu wanayoizunguka.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka TAMISEMI Juma Madaha ambaye pia ni Mchumi amesema lengo mahsusi la kikao hicho ni kuhakikisha wanaimarisha utendaji kazi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kutoka na maazimio ya kutekeleza Mkakati ambao umetungwa na Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Mazingira.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.