Programu ya urasimishaji wa ujuzi nje ya mfumo rasmi imezinduliwa kwa mara ya kwanza Mkoani Morogoro katika Gereza la Mtego wa Simba, ambapo wafungwa 201 wamehitimu mafunzo mbalimbali ya ufundi, ukiwemo ujenzi na kutunukiwa vyeti vya ujuzi huo.
Uzinduzi huo umefanyika Machi 11, 2025, ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa, katika Gereza la Mtego wa Simba, lengo likiwa ni kurasimisha ujuzi wa wafungwa hao ili kubadilisha mienendo na tabia zao watakapotoka gerezani kuweza kujitegemea na kuwa tegemeo kwa jamii na taifa.
Akifafanua zaidi, Waziri Bashungwa amesema historia kubwa imeandikwa, kwani programu hiyo itawasaidia wafungwa na kusisitiza kuwa wafungwa watakaokuwa wamepata mafunzo hayo wakiwa gerezani na kupata vyeti watanufaika na mikopo ya asilimia 10, pamoja na kuwa na mfuko maalum wa kuwawezesha kujipatia mitaji pale watakapomaliza muda wao gerezani.
Sambamba na hayo, Waziri huyo amewaasa wafungwa waliopo magerezani kujifunza kwa bidii na kurekebisha tabia zao, kwani jamii inawategemea na inajengwa na wao katika misingi ya maadili mema kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amelitaka Jeshi la Magereza kutumia rasilimali walizonazo kama misitu na mashamba kuwafundisha wafungwa ujuzi wa kilimo, ili wanapomaliza vifungo vyao waweze kutumia maarifa hayo kufanya mapinduzi ya kilimo na kukuza vipato vyao na uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania CGP Jeremiah Katungu amesema mafunzo hayo yanajumuisha ufugaji, ujenzi, utengenezaji wa samani, ususi na elimu katika ngazi zote, kuanzia msingi hadi chuo.
Jitihada hizo zimekusudiwa kuwawezesha wafungwa kuwa raia wema na wenye uwezo wa kujitegemea wanapomaliza vifungo vyao magerezani.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.