JPM azindua soko, alipa jina Kingalu, awa mbogo kwa wanaojinufaisha nalo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo Februari, 11 amezindua soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro huku akitaja baadhi ya manufaa ya soko hilo kwa wananchi na kuwataka viongozi wa Wilaya na Mkoa huo kutatua kero zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo.
Mara baada ya kuzindua soko hilo, Rais John Pombe Magufuli alitembelea soko hilo na alipoingia ndani ya soko na kuongea na wafanyabiashara wa soko hilo alipokea kero mbalimbali kutoka kwao ambazo baadae alizitolea maelekezo.
Dkt. Magufuli amesema, Soko hilo ni moja ya masoko 22 ya aina hiyo yanayojengwa na Serikali hapa nchini na kati yake, masoko tisa yamekamilika na kwamba masoko hayo yana manufaa kwa wananchi.
Rais Magufuli amebainisha manufaa ya soko hilo kuwa ni pamoja kuwarahisishia wakulima na wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa urahisi zaidi, kutoa ajira za moja kwa moja 2,500, wananchi kujipatia huduma mbalimbali yakiwemo mahita ya kila siku pamoja na Serikali kukusanya kodi kwa kwa ajili maendelo ya wananchi wenyewe.
Hata hivyo Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekerwa na uwepo wa kero nyingi za soko hilo ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wasio waaminifu kuhodhi vizimba vya soko hilo na kuvifanyia biashara kwa kukodisha shilingi elfu hamsini badala ya shilingi elfu ishirini ambayo ni kodi halali iliyopangwa na Halmashauri.
Kwa sababu hiyo amewataka wale wote waliojimilikisha vizimba na kuvikodisha kwa bei ya juu wahakikishe wanazirudisha fedha zote kwa wananchi waliokodi vizimba hivyo na kwamba hali hiyo asingpenda ijitokeze tena ndani ya soko hilo huku akitaka soko hilo lisitumike kutatua kero zao.
“Basi uzuri wa soko hili, uendane na uzuri wa kazi nzuri zinazofanywa ndani ya soko hili, lisiwe soko la kero, liwe soko la Amani” aliagiza Dkt. Magufuli
Hata hivyo amewataka Viongozi wa Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Viongozi wengine kuhakikisha wanatatua kero zote za wafanyabiashara wa soko hilo ndani ya wiki moja huku akimuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo kusimamia agizo hilo kutekelezwa.
Katika hatua nyingine Dkt. John Pombe Magufuli ametoa jina la soko hilo la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuitwa soko la Chifu Kingalu kwa lengo la kuenzi na kudumisha heshima ya Chifu huyo wa kabila la Waluguru kwa kazi nzuri alizofanya ndani ya Mkoa wa Morogoro ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo (MB) amesema soko la Chifu kingalu lina manufaa kwa wanamorogoro wote wakiwemo watu wa hali ya chini na kwamba hilo ndilo ndio lilikuwa lengo la Mhe. Rais.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare alipopata nafasi ya kutoa salamu za Mkoa pamoja na mambo mengine alimwomba Mhe. Rais kujengwa barabara ya Bigwa hadi Kisaki kwa kiwango cha lami na kumalizia ujenzi wa barabara inayosuasua ya kutoka Mikumi hadi Ifakara.
Aidha, alimwomba Rais Magufuli kujengewa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili Hospitali inayotumika sasa kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ibaki kutumika kama Hospitali yaHalmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro kusini Mhe. Innocent Kalogeresi naye alipata wasaa wa kutoa salamu za Chama ngazi ya Mkoa.
Pamoja na kumpongeza Rais kushika kiti cha Urais kwa mara ya pili Mhe Kalogeresi amewasilisha ombi la kujengwa barabara za Bigwa hadi Kisaki na barabara inayokwenda Wilaya ya Malinyi kwa kiwango cha lami.
Soko kuu la Chifu Kingalu kama linavyoitwa sasa ni moja ya masoko 22 yanayojengwa na Serikali ya awamu ya tano kama miradi ya kimkakati ambayo tisa kati ya hayo yamekamilika likiwemo soko Kuu la Chifu Kingalu ambalo hadi kukamilka kwake limegharimu zaidi ya shilingi Bil. 17.6.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.