Rais mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ameitaka Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kupinga ukatili hapa nchini.
Mhe. Kikwete amesema hayo Januari 23, mwaka huu wakati akifungua kikao cha kamati kuu cha JMAT kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Morena iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi, Mhe. Jakaya Kikwete amesema ukatili huo hususan kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ni changamoto inayohitaji mshikamano wa kijamii na elimu ya kina ili kuutokomeza kupitia kampeni za kitaifa, huku akibainisha kuwa JMAT inao uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko kwa kuunganisha nguvu za viongozi wa kidini, vyombo vya habari na wananchi wenyewe.
"Tunahitaji kuhakikisha kuwa imani potofu na vitendo vya kikatili vinakemewa kwa nguvu zote ili kudumisha heshima ya kila binadamu." Amesema Mhe. Jakaya Kikwete
Sambamba na hayo, Rais huyo mstaafu ameipongeza JMAT kwa kazi kubwa ya kuimarisha amani na mshikamano wa Taifa na kuwahimiza kuendelea kufanikisha malengo yao kwa kushirikiana na Serikali na taasisi nyingine ili kuhakikisha kuwa haki, usalama na utu wa kila Mtanzania vinaheshimiwa bila kujali tofauti zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima kwa niaba ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Peter Pinda ambaye ndiye mlezi wa JMAT Taifa, amewapongeza JMAT kwa kuendeleza na kudumisha falsafa ya 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anahimiza masuala ya maridhiano, ustawi wa kijamii, maendeleo ya rasilimali watu, na utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo, Mhe. Adam Malima ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na ushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa taifa.
Awali, Mwenyekiti wa JMAT Taifa, Alhaji Dkt. Mussa Salim, amesema kuwa JMAT si chombo cha kidini bali ni Jumuiya inayosimamiwa na viongozi wa dini, kwani kila mtu ana dini yake kwani baadhi ya Watanzania wana dhana potofu kwamba Jumuiya hiyo inalenga kuanzisha dini mseto, jambo ambalo si sahihi.
Pia, Dkt. Salim amebainisha kuwa Watanzania wote ni ndugu, na udugu huo unapaswa kuunganisha na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo ujenzi wa miradi kama zahanati, misikiti, makanisa, uchangiaji wa damu salama, kutembelea watoto yatima na kuiombea serikali ili iendelee kutunza na kudumisha amani hapa nchini.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.