Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kesho tarehe 7 Julai, 2021 anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Morogoro akitokea Jijini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela imeeleza kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan atawasili Wilayani Gairo saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya kuwasalimia na kuzungumza na wananchi wa Gairo na saa 8:00 alasiri atawasili eneo la Dumila Wilayani Kilosa ambapo pia atazungumza na wananchi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Shigela amesema majira ya saa 10:00 jioni Mhe. Samia Suluhu Hassan atapokelewa Manispaa ya Morogoro eneo la kituo kikuu cha mabasi yaendayo Mikoani cha Msamvu ambapo atazungumza pia na wakazi wa Halmashauri hiyo pamoja na maeneo jirani.
Siku ya pili, yaani tarehe 8 Julai, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan atafungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Kikristu Tanzania – CCT ambao ndio Mkutano Mkuu wa Maaskofu wote wa Jumuiya ya Kikristu utakaofanyika Mkoani hapa.
Wananchi wote wa maeneo yaliyotajwa hapo juu ikiwa ni pamoja na Gairo Mjini, Dumila na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro mnahimizwa kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais wetu ikizingatiwa kuwa hii ni ziara yake ya kwanza kuja Morogoro tangu ashike wadhifa huo wa Urais.
NB. Bonyeza link hapa chini kuona habari hii katika youtube channel yetu. please subscribe, share, like and comment.
https://www.youtube.com/watch?v=GekZ17DwNEY
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.