Rais Samia atambua mchango wa Taasisi za Kidini, azitaka kutoa Elimu ya Covid 19, Sensa ya watu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Taasisi za Kidini zina mchango mkubwa katika kuijenga nchi na kuzitaka kuendelea kushirikiana na Serikali katika azma yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema hayo Mjini Morogoro leo Julai 8, 2021 wakati akifungua Mkutano wa 31 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) uliofanyika katika Ofisi za Taasisi hiyo zilizoko eneo la Kilakala katika Manispaa ya Morogoro.
Amesema Viongozi wa dini kupitia nafasi zao wana wajibu wa kutoa elimu kwa watanzania kuhusu janga la maradhi ya Uviko – 19 ambayo bado ni tishio hapa Duniani kwa kuwataka waumini wao kufuata kikamilifu maelekezo ya kitaalamu yanayotolewa na wataalamu wa Afya.
Aidha, amewaeleza watanzania zoezi la sense ya watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwakani, zoezi ambalo amesema linawezesha nchi kupata takwimu halisi ya watu na kupelekea serikali kutambua mahitaji ya nchi na wananchi wake yaani kuweka malengo pamoja na mipango ya maendeleo.
“Hivyo basi niwasihi sana viongozi wa dini kuwahimiza wananchi kuachana na imani potofu na kushiriki zoezi hili muhimu la kitaifa” amesisitiza Mhe. Rais.
Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu wa CCT mara baada ya kufungua Mkutano wao wa 31, leo Julai 8, 2021 Morogoro
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristu Tanzania – CCT Askofu Dr. Alinikisa Cheyo, pamoja na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwavusha watanzania katika kipindi kigumu cha msiba wa Taifa kutokana na Kifo cha hayati Dkt. John Pombe Magufuli, amepongeza pia kwa uongozi wake unaojali Utawala Bora, haki za Binadamu na kufungua milango kwa lengo la kuongeza Uchumi wa nchi.
Hata hivyo, Dr. Alinikisa alimuomba Mhe. Rais kuwaondolea changamoto Jumuiya hiyo, ugumu wa kupata vibali vya kazi na vya kuishi vya wafadhiri wao kutoka nje ya nchi wanaoingia hapa nchini kwa ajili ya kutoa misaada ya kitaalamu kwa manufaa ya Taasisi ya CCT na watanzania wote kwa jumla.
Baadhi ya Maaskofu na wshiriki katika Mkutano wa 31 wa CCT uliofunguliwa na Mhe. Rais leo Julai 8, 2021
Awali, akimkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, pamoja na mambo mengine, alibainisha dhamira na mchakato wa Serikali wa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Amesema, lengo la Kujenga Hospitali hiyo ni utekelezaji wa dhamira ya Mhe. Samia Suluhu Hasaan na Seriakli yake ya awamu ya sita kutoa kipaumbele kwa Afya ya Mama na Mtoto ambapo kwa siku za karibuni ametoa zaidi ya shilingi 500 Mil. kujenga Hospitali ya Wilaya ya katika Halmashauri ya Mlimba Wikayani Kilombero, huku akibainisha umuhimu wa Mkoa huo kuwa na Hospitali ya Rufaa kutokana na mahali ulipo.
Amesema, Mkoa wa Morogoro upo katikati ya Dar es Salaam na Dodoma miji yenye shughuli nyingi, na kwamba kuna uhitaji wa Hospitali kubwa ya Rufaa itakayosaidia kutoa huduma za Afya kwa wananchi wa maeneo hayo na wa Mikoa mingine ikiwepo ya Nyanda za juu, Mikoa ya Kanda ya kati na mikoa ya ukanda wa Pwani ikiwemo ya mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Mhe. Samia Suluhu Hassan amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Morogoro huku akiweka matumaini makubwa ya kurudi kufanya ziara ya kikazi kwa kutembelea Wilaya zote za Mkoa huo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.