Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaagiza Wakuu wa Mikoa ya Pwani na Dar es salaam pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dar es salaam (DAWASA) kufanya ukaguzi na kuwaondoa wavamizi wote wa vyanzo vya maji ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa maji katika Mikoa hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi na viongozi waliohudhuria kwenye Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo Novemba 1 mwaka huu wakati akifungua Mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia ambapo kitaifa unafanyika katika ukumbi wa mikutano wa J.K. Nyerere jijini Dar es salaam.
Akifafanua zaidi Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema upungufu wa maji katika mto Ruvu unachangiwa na ukame unaotokana na shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji kama vile ukataji wa misitu kwa ajili ya kilimo na kuni, kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa samaki katika mabwawa shughuli ambazo kwa kiasi fulani zimesababisha baadhi ya mito kukauka.
“...sasa Mkuu wa Mkoa Dar es salaam na Pwani, lakini pia na DAWASA nataka muhakikishe kwamba mmekwenda na mmmehakikisha zile ‘blocks’ zote zilizopo kwenye mito zimeondoka...” amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wao Wadau wa Sekta ya Nishati Mkoani Morogoro wameshauri uimarishaji wa utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji na kupata nishati safi ya kupikia kupitia umeme wa maji hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa (wa nne kutoka kulia) akiwa pamoja na viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya wakishiriki Mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia katika ukumbi wa mikutano Hoteli ya Morena, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akitoa ushauri huo Mhandisi Jane Kadoda kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) Kanda ya Morogoro-Rufiji amesisitiza watanzania kutunza vyanzo vya maji ili kuongeza kiwango cha maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere na hivyo nishati safi ya kupikia kupitia umeme ipatikane na iwe endelevu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amesema kuna haja ya kusimamia sheria zilizopo sasa au kuziongezea makali katika kulinda mazingira, kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za kibinadamu zinazoharibu mazingira ikiwemo uchomaji wa mkaa na ufugaji mifugo mingi kupita kiasi.
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Mkoa ameshauri kamati itakayoundwa ambayo imeagizwa na Mhe Samia Suluhu Hassan iweze kutembelea visiwa vya Pemba kwa lengo la kujifunza namna bora ya kutunza mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle akitoa mchango wake kuhusu mijadala ya kuboresha nishati safi ya kupikia.
Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Albert Msando akichangia hoja kwenye mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya Kupikia.
Akichangia hoja hiyo ya mjadala wa Nishati safi ya kupikia Fatma Mwassa amefafanua kuwa Mkoa wa Morogoro utakuwa shamba la mazao ya matunda na viungo mbalimbali vikiwemo karanga miti, hiriki, mdarasini na Karafu.
Mjadala wa wadau wa nishati umelenga kujadili namna bora ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia isiyo na athari kwenye mazingira kama vile matumizi ya nishati ya gesi na umeme.
Mjadala huo unatarajia kuendelea Novemba 2 mwaka huu, huku mikoa ya Dodoma, Iringa, Tabora, Shinyanga na Morogoro ikishiriki mubashara kwa njia ya mtandao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.