Wakazi wa Kijiji cha Changarawe Kata ya Masanze wilayani kilosa Mkoani Morogoro wamempongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajengea Kituo cha Afya kinachotarajiwa kwenda kuokoa vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.
Bwana Jonathan Wilson Diwani Kata ya Masanze akitoa pongezi mbele ya Mkuu wa Mkoa.
Pongezi hizo zimetolewa na wananchi wa Kijiji cha Changarawe Oktoba 5 mwaka huu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa aliyoifanya Wilaya Kilosa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilayani humo ukiwemo mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Masanze.
Muonekano wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha Afya Masanze Wilayani Kilosa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho wamesema wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kwenda kufuata huduma ya Afya Mjini Kilosa huku baadhi ya wajawazito wakipoteza maisha kutokana na kuchelewa kufika maeneo ya kutolea huduma ya Afya.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akizungumza na wananchi wa Masanze Wilayani Kilosa
Miongoni mwa wakazi wa Kata ya Masanze akiwemo Bi. Evalina Moreli, amesema kuwa kabla ya kituo hicho kujengwa wananchi walikuwa wanatembea umbali wa zaidi ya kilometa 20 kufuata huduma ya matibabu Mjini Kilosa ambapo watoto chini ya miaka 5 na wajawazito wamekuwa wahanga wakubwa kutokana na ukosefu wa kituo cha Afya, kwa sasa wanamshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajengea kituo hicho cha Afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dkt. Mamisa Basike amesema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha Masanze ambacho wanategemea kitaokoa maisha ya wajawazito na watoto kundi ambalo limekuwa na changamoto ya kuhatarisha maisha yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaj Majid Mwanga akitoa shukrani zake kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akizungumza na wananchi mbele ya Kituo hicho cha Afya ameiagiza kamati ya Ujenzi ya Kituo hicho cha Afya pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa majengo yaliyobaki na kuhakikisha yanapata vifaa tiba ili matumizi ya majengo hayo yaanze mara moja.
“.... sasa tukamilishe majengo yote yaliyoanzishwa mpaka yafike mwisho, lakini cha pili tuweke vifaa tiba majengo yote yaliyokamilika ili matumizi yake yaanze mara moja....” amesema Fatma Mwassa.
Kufuatia changamoto za Afya zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Kata ya Masanze, Serikali hadi sasa imekwisha peleka fedha zilizotengwa kwa ujenzi wa kituo hicho cha Masanze ambazo ni shilingi milioni 500.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.