Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanueli Kalobelo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuongeza kasi na usimamizi wa ukusanyaji wa Mapato ya ndani ili Halmashauri hiyo iweze kujitegemea katika utendaji kazi wake kwa kuwa ina fursa ya vyanzo vingi vya mapato ndani ambavyo bado havijaibuliwa.
Mhandisi Kalobelo ametoa maagizo hayo hivi karibuni wakati akifungua kikao kazi cha Watendaji wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kilicholenga kutathmini utendaji kazi kwa kipindi cha robo mwaka ikiwa ni utaratibu waliojiwekea ndani ya Halmashauri hiyo ili kuiendeleza pamoja kuondoa kero zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Kilosa.
Kalobelo amesema, Halmashauri ya Kilosa ni Kongwe na ina eneo kubwa hivyo haipaswi kuwa na makusanyo madogo kama halmashauri zenye maeneo madogo. Lakini pia amesema Halmashauri ina rutuba ya kutosha, ina miundo mbinu ya kitaifa kwa maana ya reli TAZARA na Mwendo kasi, ina barabara kuu zinazopita ndani ya Halmashauri hiyo kuelekea Mikoa ya nyanda za juu kusini na mikoa ya kaskazini mwa nchi hii, ina hifadhi ya mbuga ya wanyama ya Mikumi na ina Viwanda, hivyo amesema kutokana na fursa hizo haipaswi kuwa na makusanyo kidogo kama kinachokusanywa sasa.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo mwaka 2018/2019 iliweka malengo ya kukusanya Tsh. 3.7 Bil. na kufanikiwa kukusanya Tsh. 2.7 Bil. sawa na 74%. Mwaka 2019/2020 ilipanga kukusanya shilingi 5.2Bil. na ikakusanya shilingi 3.8 Bil. sawa na 72% na mwaka 2020/2021 imepanga kukusanya Tsh. 5.1Bil. na hadi Disemba ilikuwa imekusanya shilingi 1.3Bil. sawa na 25% hali ambayo amesema haioneshi kufikia malengo kwa kuwa kwa kwa sasa ilibidi iwe imefikisha zaidi ya asilimia hamsini. Hata hivyo amesema nje ya kuweka makisio madogo ya ukusanyaji wa mapato hayo ya ndani ukilinganisha na utajiri uliopo ndani ya Halmashauri hiyo, bado makisio hayo hayakusanywi kwa asilimia zote kama ambavyo walikisia.
Kwa sababu hiyo, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale kuwa mkali kwa watendaji wake katika eneo hilo la ukusanyaji wa mapato huku akimtaka katika kikao hicho suala la ukusanyaji wa mapato iwe agenda itakayotoka na maazimio, kwa kila Mtendaji kuhakikisha anakwenda kuibua chanzo cha mapato ya ndani lakini ambacho hakileti kero kwa wananchi.
“sasa hapa Mkurugenzi tusioneane aibu, hakikisha kila mtu anakwambaia mimi lengo langu ni hili makusanyo yangu ni haya… muwajibishane katika ukusanyaji wa mapato” aliagiza Mhandisi Kalobelo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo amewataka Watendaji wote wa Halmashauri hiyo kutatua kero za wananchi katika maeneo yao badala ya kuwafanya kufunga safari kwenda Wilayani ama Mkoani kutatua kero zao wakati wao kama watendaji wa Serikali wapo. Ameongeza kuwa kuishi maadili ya utumishi wa Ummaitasaidia wao kuaminika kwa wananchi na hivyo watawapelekea kero zao ili kuzitatua.
Mwisho, Katibu Tawala amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Asajile Mwambambale kwa ubunifu wake wa kuanzisha utaratibu wa kuwa na kikao cha pamoja na watumishi wake kwa kila robo ya mwaka ili kutathmini utendaji wao wa kazi jambo ambalo amesema ni la kuigwa na halmashauri nyingine za Mkoa huo kwa kuwa linalenga kuleta maendeleo ya watu, Halmashauri, Mkoa na Taifa kwa jumla.
Kwa upande wa Mbunge wa jimbo la Mikumi Mhe. Dennis Londo amewataka watumishi halmashauri hiyo wawe sehemu ya majibu ya kero za wananchi na wakishindwa basi waepuke kuwa sehemu ya kero za wananchi, huku Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na kupokea maelekezo ya Katibu Tawala wa Mkoa na kuyafanyia kazi, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kuwa na kariba ya kuwasikiliza wananchi kwa upole pale wanapotoa kero zao.
Nao watendaji wa halmashauri hiyo wakiwemo Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata pamoja na Watendaji wa Vijiji wameahidi kila mmoja kwenda kuyafanyia kazi maelekezo ya Katibu Tawala wa Mkoa hususana katika suala nzima la uibuaji wa vyanzo vya mapato huku wakishukuru utaratibu huo wa kuwa na vikao vya pamoja kwa kila baada ya miezi mitatu au robo mwaka.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.