Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewaagiza wataalamu wa kilimo, afya na walimu wa shule za msingi na sekondari kushirikiana vema katika maeneo yao ili kuwa na mpango utakaozisaidia shule kupata vyakula vya kuwalisha wanafunzi wa madarasa yote ili kujenga afya na kuongeza umakini darasani.
Dkt. Mussa ametoa agizo hilo Oktoba 25, Mwaka huu wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea shule za Msingi na Sekondari zilizopo Mkoani humo akitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga lengo likiwa ni kuangalia hali ya lishe mashuleni.
Akifafanua zaidi, Dkt. Mussa amesema shule nyingi zina maeneo makubwa ambayo wanaweza kushirikiana na maafisa kilimo kulima mazao mbadala ya kimkakati hususan michikichi, kokoa na mikarafuu na kubainisha kuwa miche ya mikarafuu 40 inaweza kuleta faida ya shilingi milioni 9 ndani ya miaka minne, hivyo shule inaweza kujiendesha yenyewe na kutoa chakula kwa wanafunzi bila ya usaidizi kutoka kwa wazazi.
"... suala la lishe ni la wote ninyi watu wa kilimo, walimu, watu wa afya na wengine wengi lazima tuungane pamoja ili tuweze kufikia lengo..." Ameagiza Dkt. Mussa Ali Mussa
Aidha, Dkt. Mussa amekemea vikali wanafunzi kula chakula cha aina moja hususan makande na ugali bila mboga mboga wala matunda kwani amesema chakula cha aina moja hudumaza afya ya akili na mwili kudhoofika.
Sambamba na hayo, Katibu Tawala huyo wa Mkoa amezipongeza Shule za Sekondari za Celina Kombani na Msogezi kwa kuanzisha mpango mkakati wa wanafunzi wa vidato vyote waliopo shuleni kupata chakula chenye lishe bora na kutaka shule hizo kuwa mfano ili shule zingine kwenda kujifunza.
Kwa sababu hiyo, Dkt. Mussa amempandisha cheo aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Msogezi Mwl. Zena Idd Salum kwa kutafuta ufumbuzi wa wanafunzi wa madarasa yote kula mlo kamili kwa kulima mazao ya asili ikiwemo mihogo na mbaazi kwa ajili ya wanafunzi kula shuleni.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Richard Magoma amefurahishwa na utendaji kazi wa aliyekuwa Kaimu Mkuu wa shule ya Sekondari ya Msogezi na kuwataka walimu wakuu kuwa mfano katika uchangiaji wa chakula na kutawajenga wanafunzi kuwa na ushirikiano wa kula chakula kwa pamoja kuepuka vyakula vya kununua migahawani.
Naye, Afisa lishe wa Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amesema shule zinapaswa kuanzisga vitalo vya kulima mboga mboga pamoja na kulima mazao jamii ya mikunde na mbaazi na kutoa vyakula vya aina nyingi hususan vinavyozingatia lishe bora kama wanga, protini na vitamini ili kupata wanafunzi mahiri ambao ndio wataalamu wa Taifa la kesho.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.