Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewaagiza watendaji wa Serikali Mkoani humo kuhakikisha wanafunzi wote wa shule za msingi na Sekondari wanakula chakula shuleni ili kujenga afya na kuongeza umakini darasani.
Dkt. Mussa ametoa agizo hilo Septemba 2, mwaka huu wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea shule za Msingi na Sekondari zilizopo Mkoani humo akitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero lengo likiwa ni kuangalia hali ya lishe mashuleni.
Akifafanua, Dkt. Mussa amesema, hadi sasa wanafunzi wanaokula chakula shuleni ni wachache badala yake wengi wananunua vyakula kwa fedha zao hali ambayo si salama kwa Afya zao huku wengine hula baada ya kurudi nyumbani kwao.
Kwa sababu hiyo, Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka Viongozi wa shule zote hususan watendaji wa Serikali kutumia mbinu mbadala kuzungumza na wazazi ili kuchangia chakula au fedha ili kuhakikisha wanafunzi kupata chakula kikiwa na mboga mboga pamoja na matunda.
"... ni lazima wanafunzi wote wale shuleni kwa njia yoyote tutakayokubaliana kati yetu na wazazi..." Ameagiza Dkt. Mussa Ali Mussa
Aidha, Dkt. Mussa amekemea vikali wanafunzi kula chakula cha aina moja hususan makande na ugali bila mboga mboga wala matunda kwani amesema chakula cha aina moja hudumaza afya ya akili na kusababisha ufaulu kushuka darasani.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mussa ametaka kila shule kuhakikisha inalima mboga mboga na mazao ya biashara kama mishelisheli na mikarafuu ili shule hizo ziweze kujitegemea kiuendeshaji.
Kwa upande wake, Afisa lishe wa Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe ameishauri Kamati ya Shule ya msingi ya Dibamba kuwa na vyakula vya aina nyingi hususan vinavyozingatia lishe bora kama wanga, protini na vitamini ili kupata wanafunzi mahiri ambao ndio wataalamu wa Taifa la kesho.
Naye, Afisa Afya wa Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Laurent Gallet amewasisitiza walimu kuhakikisha wanasimamia usafi katika maeneo yote ya shule ukiwemo usafi wa vyoo, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuchemsha maji ya kunywa na kutenga vifaa vya kuhifadhia taka hali itakayosaidia hivyo kutasaidia kuepusha magonjwa ya kuambukiza.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.