Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amebaini sababu za kushuka kwa ufaulu katika shule za Msingi na Sekondari ikiwemo changamoto ya kutopatikana kwa lishe bora hali inayochochea ufaulu kuwa wa wastani Mkoani humo.
Dkt. Mussa amesema hayo Agosti 28, mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea shule za Msingi na Sekondari zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa lengo la kuangalia hali ya lishe mashuleni.
Akifafanua zaidi Dkt. Mussa amesema wanafunzi wanaokula chakula cha aina moja mashuleni hususan makande, ugali na wali bila mboga za majani wala matunda hudumaza afya ya akili na kusababisha ufaulu kushuka darasani.
"... matokeo sio mazuri kwa sababu huku chini hawali vyakula vyenye lishe ambapo wanadumaza afya zao..." amesema Dkt. Mussa Ali Mussa
Kwa sababu hiyo, Katibu Tawala huyo amewataka Maafisa Kilimo wa Halmashauri hiyo kushirikiana na Walimu kuotesha vitalu vya mboga mboga kwa kutumia mbolea na mbegu za kisasa ili kupata mboga zitakazotumika wakati wa chakula.
Pia, amewataka walimu kubaini mboga za asili zilizopo maeneo husika zikiwemo mchunga, mbwembwe, mnafu, kisamvu, majani ya kunde na mgagani kuzichuma na kuzikausha ili kuzitumia mashuleni wakati wa kiangazi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma amewashauri walimu pamoja na kamati za shule kubaini wanafunzi wenye mahitaji maalum na kupewa kipaumbele katika huduma za chakula ili kupata usaidizi pale wanapohitaji msaada.
Nae, Afisa Afya wa Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Laurent Gallet amewasisitiza walimu pamoja na kamati za usafi za shule kuhakikisha wanafanya usafi katika maeneo yote ya shule ukiwemo usafi wa vyoo, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kuchemsha maji ya kunywa na kutenga vifaa vya kuhifadhia taka hali itakayosaidia wanafunzi kuepukana na magonjwa ya kuambukiza.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.