Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameendelea kuhamasisha kampeni ya "Jisomeshe na Mkarafuu" kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na wakazi wote wa Wilayani Mvomero, ikiwa na lengo la kuwawezesha wanafunzi hao kiuchumi kupitia kilimo cha mkarafuu na kujisomesha kupitia kilimo cha zao hilo.
Akizungumza wakati wa zoezi la kugawa miche hiyo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule za sekondari za Kipera na Homboza Machi 14, 2025 Dkt. Mussa amesema Viongozi wa Mkoa wa Morogoro wameanzisha kampeni hiyo kama mkakati wa kuwaandaa vijana kwa maisha ya baadaye kwa kuwawezesha wanafunzi hao kujiendeleza kimasomo kupitia zao hilo.
Ameongeza kuwa miche hiyo wanapewa wanafunzi hao bila malipo wakapande katika maeneo yao kwenye mashamba yao ama ya wazazi/ walezi wao na si kwenda kupanda mashamba au maeneo ya shule na kwamba kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza atapewa miche 10 na kuwataka waitunza ili iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
"...nyie wanafunzi wa form one, tunataka kila mwanafunzi mmoja leo hii, tumuachie miche ya mikarafuu kumi... miche hii isiwe mali ya shule mkaipande kwenu..." amesisitiza Dkt. Mussa
Kwa mujibu wa Katibu Tawala huyo, kwa sasa bei ya kilo moja ya karafuu ni shilingi 20,000/= hivyo, mche mmoja una uwezo wa kuzalisha kilo tano huku akisema kuwa kwa miche hiyo 10 itazalisha kilo 50 ambazo ni sawa na shilingi 1,000,000/= hivyo, kupitia zao hilo wanafunzi wataweza kujigharamia masomo yao kupitia zao la mkarafuu.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira amesema kapeni hiyo ilizinduliwa rasmi Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, na inaendelea kutekelezwa halmashauri zote za Mkoa huo na sasa wako Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, huku akiwataka wanafunzi kuipokea kampeni hiyo ambayo itawasaidia kutimiza ndoto zao.
Naye, Mwl. Isakwisa Asesisye akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amemshukuru Katibu Tawala huyo kwa kuanzisha kampeni hiyo ndani ya Mkoa huo na sasa iko Mvomero Halmashauri yenye jumla ya shule za sekondari 37 ambapo kwa kuanzia kampeni hiyo imeanza kwa shule za Homboza na Kipera.
Nao Wanafunzi waliopatiwa miche hiyo wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema kuwa utapunguza changamoto za ada na mahitaji mengine kwao lakini pia kampeni hiyo itawajengea misingi ya kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea.
Jumla ya wanafunzi 473 wa shule za Sekondari ya Kipera na Homboza wamepatiwa jumla ya miche 4730 ya karafuu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.