RAS MOROGORO AENDELEZA MOTO WA KILIMO CHA MAZAO YA KIPAUMBELE.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameendelea na kasi ya kutoa ushauri wa bure kwa wananchi wa Mkoa huo kulima mazao ya kipaumbele likiwemo zao la Karafuu, kwa lengo la kuongeza kipato chao, Mkoa, Taifa Pamoja na utunzaji wa mazingira.
Dkt. Mussa amesisitiza na kutoa ushauri huo Mei 9, mwaka huu 2024, wakati wa zoezi la kugawa miche 300 ya karafuu katika kata ya Mzumbe kijiji cha Tangeni Wilayani Mvomero Mkoani humo.
Mara baada ya zoezi hilo Kiongozi huyo ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali Mkoani humo amewashauri wananchi pasi na kuwalazimisha, kukubali kulima zao la karafuu kwa kuwa litawainua kiuchumi na kuwaongezea kipato na kutunza mazingira yao.
" ... Sote tuweze kukubali kupanda karafuu katika maeneo yetu na ukweli sio karafuu peke yake, sehemu inayoota karafuu otesha karafuu, sehemu inayoota michikichi otesha michikichi, sehemu inayoota kahawa otesha kahawa na sehemu inayoota parachichi otesha parachichi ...." amesisitiza Dkt. Mussa.
Amesema, lengo la Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha inawawezesha wananchi wake ili wabadilike na Maisha yao kuwa katika hali nzuri kwa kuongezeka kipato chao kupitia kilimo cha zao la karafuu.
katika hatua nyingine Dkt. Mussa amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inaendelea na jitihada za kutafuta masoko kwa ajili ya kuuza mazao ya Iliki, karafuu, vanila na mdalasini ambapo hadi sasa wameweza kupata soko la mazao ya karafuu na Iliki.
Akionesha shauku ya kuwainua wananchi wa Tangeni kiuchumi, Dkt. Mussa ameahidi kugharimia ziara ya mafunzo Kwenda baadhi ya maeneo ya Mkoa huo ambayo tayari wanalima zao hilo ili kujifunza na kuona uhalisia wa faida ya zao hilo la karafuu.
“…….Gari bure vile vile chakula mtakachokwenda kula kule bure, nyie mkubali tu Kwenda kuona wenzenu wanavyofaidika….” ameahidi Dkt. Mussa.
Akimkaribisha Katibu Tawala huyo kuongea na wananchi wa Tangeni kabla ya ugawaji wa miche hiyo, Katibu Tawala Msaidizizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira amewataka wananchi wa Tangeni na vijiji Jirani kupokea miche hiyo, kuipanda na kuitunza kwa manufaa yao na ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa Wilaya ya Mvomero Bi. Consolata Tarimo amesema hadi sasa wamekwishagawa miche 1000 ya karafuu ambapo miche 200 wamegawa katika kijiji cha Manza, miche 300 kijiji cha Tangeni na miche 500 wameigawa kwa wananchi wa kata ya Bunduki.
Aidha, Bi. Consolata amebainisha uwepo wa kitalu chenye miche 12000 ya karafuu kilichopo kata ya Mhonda ambayo wamepanga kuigawa kwa wananchi wa kata mbalimbali, matarajio ni kwamba baada ya miaka mitano zao hilo litainua kipato cha wananchi wa Wilaya hiyo.
Nao wananchi wa Kijiji cha Tangeni akiwemo Bw. Mustafa Salum, Pamoja na kuishukuru Serikali ngazi ya Mkoa kuwapelekea zao la karafuu, bado wameomba kupewa mafunzo na Elimu ya namna ya kustawisha na kutunza miche ya zao hilo huku wakiomba mbegu kwa ajili ya kuotesha miche ili zao hilo liwe endelevu.
Ili kuondokana na changamoto ya uharibifu wa mazingira hususan ya ukataji hovyo wa miti, Mkoa wa Morogoro umekuja na njia mbadala ya kulima mazao ya Karafuu, kahawa, mchikichi, Parachihi na Kakao kama njia ya kutunza mazingira lakini pia kuongeza kipato kwa wananchi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.