Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, ametoa wito kwa watendaji wa Serikali kushirikiana pamoja ili kuhakikisha mafanikio ya programu ya usalama wa mtoto mtandaoni yanafikiwa.
Dkt. Mussa ametoa kauli hiyo Machi 14, 2025, wakati akifungua mafunzo kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Mussa amesema Serikali imeanzisha programu mbalimbali za kusaidia wananchi, lakini utekelezaji wake umekuwa na changamoto kutokana na ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa watendaji wa Serikali.
"Kila mmoja anafanya kazi kivyake, kila mmoja anaona kwamba hili linamwenyewe, sio la kwangu, naomba mshirikiane" alisema Dkt. Mussa.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Usalama Mtandaoni na Uchunguzi wa Makosa ya Kidigitali, Bw. Yusuph Kileo, amesema asilimia 87 ya mitandao ya kijamii inachangia mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii. Amesisitiza kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti za kulinda watoto dhidi ya ukatili na changamoto za kiusalama mtandaoni kupitia programu hiyo mpya.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Mwelinde Katto, amefafanua kuwa tafiti zinaonyesha asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wanatumia mitandao ya kijamii, huku asilimia 4 wakikutana na wahalifu mtandaoni na asilimia 5 wakilazimishwa kutuma picha za utupu.
Bi. Mwelinde ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa watoto, wazazi, walimu, na jamii kwa ujumla kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni. Mafunzo hayo yanatolewa kwa wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Wakuu wa Dawati la Jinsia la Polisi, na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, na Dodoma.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.