RAS Morogoro akabidhi pikipiki kwa Maafisa wa Bonde, ataka zitumike kwa malengo kusudiwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewaagiza watendaji wa vijiji na Kata kuwa ni sehemu ya jumuiya za watumia maji zinazoendeshwa katika maeneo yao ili kulinda maslahi ya wananchi waliopo katika maeneo hayo hususan vyanzo vya maji.
Mhandisi Kalobelo ametoa agizo hilo Novemba 24 mwaka huu katika hafla fupi ya kukabidhi Pikipiki 18 kwa watumishi wa jumuiya ya Wasimamizi na Waratibu wa utunzaji wa vyanzo vya maji katika Bonde la Wami Ruvu iliyofanyika katika Ofisi za Afisa Maji Bonde la Wami Ruvu zilizoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhandisi Kalabelo amesema jumuiya hizo zimeanzishwa kisheria na serikali kwa ajili ya ufuatiliaji na usimamizi wa rasilimali maji na kuhakikisha sheria zote zinazohusu maji zinalindwa kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji kwa maslahi ya wananchi.
Amesema imejijitokeza hivi karibuni Maafisa wa Bonde wanapokuwa na changamoto za ukiukwaji katika kutuza vyanzo vya maji na kuzifikisha changamoto hizo kwa Watendaji wa vijiji au Kata watendaji hao wamekuwa wakiwajibu maafisa hao kuwa changamoto hizo haziko kwenye usimamizi wa Ofisi ya ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, jambo ambalo Mhandisi Kalobelo amewataka watendaji hao kuacha tabia hiyo mara moja.
“Mtendaji wa Kijiji, Mtendaji wa Kata upo pale kulinda na kuhakikisha kwamba sheria zote za Serikali zinatekelezwa, sasa nione na mniletee Mtendaji ambaye hatakuwa na kauli hiyo” alisema Mhandisi Kalobelo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo ametoa rai kwa wana morogoro wote kuwa wasimamizi endelevu wa utunzaji wa vyanzo vya maji kwa sababu maisha ya kila mwanadamu yanategemea uwepo wa maji.
Aidha, amesema usimamizi wa rasilimali maji unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo shughuli za kilimo kandokando ya mito, ukosefu wa usafiri na shughuli za Kilimo hali inayopelekea upungufu wa maji ndani ya Mkoa.
Akikabidhi Piki piki hizo kwa watumishi wa jumuiya ya Wasimamizi na Waratibu wa utunzaji wa vyanzo vya maji katika Bonde la Wami Ruvu, Mhndisi Kalobelo amewataka Maafisa hao kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na yule atakayetumia pikipiki hizo tofauti na malengo (kama bodaboda) atafikishwa mahakamani na hatua za kiutumishi dhidi yake zitachukuliwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Morogoro – MORUWASA Julius Tanika amesema mahitaji ya maji kwa sasa katika Manispaa ya Morogoro ni Meta za ujazo 67,000 kwa siku, ambapo kwa miaka 10 ijayo zitahitajika Meta za ujazo 126,000 kwa siku.
Naye, Afisa maji Bonde la Wami Ruvu Simon Ngonyani amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo katik utendaji kazi wao wa kila siku ni uharibifu wa vyanzo vya maji hivyo kuna upungufu wa maji ukilinganisha na uhitaji wa maji kwa jamii iliyopo katika bonde la Wami Ruvu.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.