Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja amewataka watumishi wa Umma Mkoani humo kumpa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yake ili kuyafikia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake katika kufikia uchumi wa kati.
Bi. Mariam Mtunguja amesema hayo Juni 4, mwaka huu wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati yake na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akiongea na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakuu wa Taasisi za Umma zilizopo Mkoani humo Bi. Mariam amesisitiza ushirikiano pamoja na kuheshimiana katika kufanya kazi ili kuleta tija kwa Mkoa na Taifa.
“nawatakia kheri sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana, lakini naomba ushirikiano mimi ni dereva tu nimekaa pale. Kama gari halina mafuta haliwezi kwenda, kama halina mataili mazuri haliwezi kwenda…” amesisitiza Bi. Mariam Mtunguja.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro, kila mmoja kufikisha asilimia 100 ya makusanyo ya mapato ya ndani katika maeneo yao kabla au ifikapo Juni 30 mwaka huu.
‘’Tunaelekea tarehe 30 ya mwezi wa sita, naamimi kila Mkurugenzi amejiwekea asilimia za ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri yake, hivyo naomba mkasimamie zoezi hili kikamilifu ili tuepuke kupata hati chafu katika Mkoa wetu, Mkaguzi wa ndani hakikisha unalifuatilia hili’’ Amesema Bi. Mariam.
Kwa upande wake Mhandisi Emmanuel Kalobelo akiongea wakati wa makabidhiano hayo, amewaomba wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na watumishi wote wa Umma Mkoani humo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Bi. Mariam Mtunguja kama ambavyo walimpa yeye ushirikiano wa kweli ili kuufikisha Mkoa huo katika malengo yaliyokusudiwa.
‘’Na nafarijika kabisa, nakabidhi mkoba katika mikono salama, sina shaka na utendaji kazi wake, ni mtu ambaye namfahamu kwa muda mrefu, nimshukuru Mhe. Rais kwa kukuchagua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro. Lakini pia niombe mtoe ushirikiano wa dhati kwake ili kuufikisha Mkoa huu tulipokusudia’’ Amesema Mhandisi Kalobelo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.