Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutekeleza Mfumo wa Anwani za makazi hapa nchini na kuhimiza ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi kwa kuwa ndiyo wenye jukumu la kusimamia usalama wa raia na mali zao.
Dkt. Mussa ametoa pongezi hizo Oktoba 18 mwaka huu wakati akifungua kikao kazi cha kujadili matumizi ya mfumo wa anwani za makazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kikao hicho kimejumuisha taasisi za umma na zisizo za umma.
Katibu Tawala huyo amesema anwani za makazi zina umuhimu katika kila nyanja ikiwemo kukuza biashara, ulinzi na usalama lakini kuna haja ya kushirikisha wadau ili kuwa na uelewa wa pamoja kutokana na umuhimu wa anwani za makazi.
“...anwani za makazi zina umuhimu mkubwa sana, kwa hiyo ombi langu katika anwani za makazi washirikisheni kwa kiwango kikubwa hawa mapolisi kwa sababu wao ndiyo wanao tulinda...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa amebainisha kuwa anwani za makazi zitaisaidia serikali kukusanya mapato kutoka kwa wafanyabiashara kwa kuwa watafikika kwa urahisi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mratibu wa utekelezaji wa Mfumo wa Anwaniza Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Jampyon Mbugi amesema lengo la ujio wao ni kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuhakiki taarifa za anwani za makazi katika Halmashauri hiyo, na kubainisha kuwa zoezi hilo limekamilika.
Hata hivyo amesema Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inatakiwa kutumia taarifa hizo katika utoaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya barabara. Aidha, amesema Wizara inatarajia zoezi hilo kuwa endelevu katika Mkoa huo.
Naye, Mratibu wa Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bi. Jacqueline Mushi amesema zoezi hilo limefanyika kwa awamu tatu 2018-2019 kwa kata za Mjini, 2022 kupitia agizo la Serikali. Aidha, zoezi hilo kwa Manispaa ya Morogoro limekamilika ambapo zaidi ya asilimia 93 ya wakazi wamefikiwa kwa kata 29 za Manispaa hiyo.
Mfumo wa Anwani za Makazi ni miundombinu ambayo kwa pamoja inatambulisha mtu au kitu kilipo iwe ni ofisini, nyumbani au eneo la biashara, anwani ya makazi imeundwa na namba ya nyumba, jina la barabara na postikodi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.