RAS MOROGORO ASISITIZA USHIRIKIANO KAZINI, AAGIZA WANAOKWAMISHA WAWEKWE PEMBENI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja ametoa Wito kwa Uongozi wa Wilaya ya Gairo na Halmashauri ya Wilaya hiyo kufanya kazi kwa Ushirikiano zaidi hususani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo huku akiagiza wanaokwamisha kazi hizo za Maendeleo kuwekwa pembeni.
Katibu Tawala ametoa maagizo hayo Machi 22 mwaka huu wakati wa ziara ya siku moja Wilayani humo alipotembelea miradi ya maendeleo ya Wilaya hiyo akiambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja (Kulia)
Amesema,katika utendaji kazi anaamini palipo na ushirikiano na uwazi hakuna linaloshindikana na kuwataka watendaji wa Sekta ya Umma wa Halmashauri hiyo na maeneo mengine ya Mkoa huo kufanya kazi kwa uwazi na ushirikiano.
“na imani yangu mimi ni kwamba kama tukishirikiana na tukiambizana hakuna linaloshindikana” amesema Mariam Mtunguja.
RAS Morogoro (mbele aliyejifunika kilemba kichwani ) akikagua ujenzi wa majengo Hospitali ya Wilaya ya Gairo. mbele kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Ezron Kilamhama
Aidha, amewataka Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Gairo kutosita kuwaweka pembeni watendaji wa sekta ya Umma ambao wanakwamisha utendaji kazi wa wengine hususana katika utekelezaji wa Miradi ya maendeleo.
“Tukiona mtu anatukwamisha tunamuweka pembeni sisi tunaendelea,yaani hiyo msiogope kabisa, kumuweka mtu pembeni ni kitu cha kawaida kabisa katika Utendaji” amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Gairo
Akiwa katika ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara za mjini Gairo zilizopandishwa hadhi kutoka changarawe hadi kiwango cha lami amemtaka mkandarasi anayejenga barabara hizo kukamilisha kazi hiyo kwa wakati huku akimtaka kuanza kazi ya kuweka lami kabla ya mvua hazijaanza kunyesha.
Hata hivyo amememtaka mkandarasi wa Kampuni ya Coberg Construction Co. Limited anayepewa kazi hiyo kuhakikisha anajengea mitaro ya maji pembezoni mwa barabara hizo ili kuongeza uimara wake huku akiwataka viongozi wa Halmashauri ya Gairo kupanda miti kando ya barabara zinazojengwa ili kupendezesha Mji lakini pia mazingira yake yaweze kuendana na hadhi ya barabara hizo za Lami.
Katika Hatua nyingine Katibu Tawala huyo ametembelea ujenzi wa majengo manne yanayojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Gairo na kuagiza kuongeza mafundi wengine ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati vinginevyo fedha zake zinaweza kurudi Hazina Kuu ilhali wananchi wanahitaji huduma ya Afya.
Sambamba na hayo, amewataka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoani humo kuongeza weledi katika utendaji wao ili kuwachukulia hatua za mapema(Pro - active) wale wote watakathubutu kujihusisha na rushwa katika miradi ya maendeleo, badala ya kusubiri mambo kuharibika na miradi hiyo kusimama hivyo kuwanyima wananchi haki yao ya kupata huduma za kijamii.
Mwisho, amewapongeza Chama na Serikali Wilayani humo kwa kufanya kazi kwa ushirikiano, na kutumia fursa hiyo kwa namna ya pekee kumshukuru Mbunge wa Jimbo hilo Ahmed Shabiby kwa kujitolea kuweka taa kwa baadhi ya Barabara za lami zinazoendelea kujenngwa Mjini Gairo na kwamba wanatambua mchango wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame amemhakikishia Katibu Tawala wa Mkoa kuwa yeye pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama watahakikisha wanasimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa Wilayani humo na kukamilika kabla ya Juni mwaka huu, kwani amesema kutokamilika kipindi hicho ni tafsiri kuwa wao hawatoshi nyadhifa zao.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame (kushoto) akimpa maelezo RAS Morogoro juu ya ujenzi wa majengo ya Hospitali hiyo
Naye Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo SACP Fortunatus Musilim amesema watahakikisha wanasimamia fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika kwenye maeneo yaliyoelekezwa na si vinginevyo.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Gairo Mhandisi Masala Nkulu ameipongeza Serikali kwa kuongeza Bajeti ya TARURA mara dufu ukilinganisha na bajeti ya mwaka uliotangulia. amesema Wilaya hiyo bajeti imeongezeka kwa asilimia 250 kwa sababu hiyo amemhakikishia Katibu Tawala wa Mkoa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Amebainisha kuwa TARURA kwa Wilaya ya Gairo katika Bajeti ya mwaka 2021/2022 imepangiwa na Serikali kupewa Tsh. 2,329,880,000.00 hadi sasa Serikali imekwisha toa Tsh. 1.480,165,677.19.
Katika ziara hiyo Katibu Tawala ametembelea ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ujenzi wa Barabara ya Kichangani – Magengeni yenye urefu wa Km. 1.1 kwa kiwango cha lami ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu Tsh.540,673,616.25 na Barabara ya Ramashop – Msingisi Guest kiwango cha lami Km.43 gharama ni Shilingi 259,326,383.75.
Miradi mingine aliyotembalea ni pamoja na Ujenzi wa Mitaro na Karavati barabara ya Ukwamani kwa gharama ya Tsh.84,051,375.00, Ujenzi wa Barabara ya Ukwamani – Meshugi kwa gharama ya Tsh.205,334,275.00 pamoja na majengo manne ya Hospitali ya Wilaya yakiwemo majengo mawili ya Upasuaji kwa upande wa wanaume na wanawake, jengo la Dharura na nyumba moja ya Mtumishi.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.