Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Wakuu na Wataalam wa idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ngazi ya Mkoa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Musa Ali Musa ameelekeza kuongeza kasi ya utendaji kazi katika sehemu ya uwekezaji na biashara kutokana na kuwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia duniani kote ili kutoa huduma za uhakika na kuwezesha uchumi kukua Mkoani humo na Taifa kwa ujumla.
Alhaji Dkt. Mussa ameyasema hayo Leo Septemba 4, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha Wakuu na Wataalam wa idara ya viwanda, biashara na uwekezaji kutoka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kinachofanyika siku mbili katika ukumbi wa mikutano wa Mbaraka Mwinshehe uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji wataalam hao.
"...naamini kikao hiki kitaongeza ile chachu ya kutekeleza shughuli zake kwa kasi zaidi na mafunzo haya yakiwekwa vizuri kwa mifano halisi yatatunufaisha sisi wenyewe kwa kuwa na kasi katika utendaji pasipo kuwa na changamoto yoyote lakini pia yatawanufaisha watu wengine tuliopewa dhamana ya kuwahudumia..." Amesema Dkt. Mussa Ali Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa ameelekeza wakuu katika kikao kazi hicho kutoa mafunzo kwa wataalam ili kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza hapo mwanzo zikiwemo kwenye Stakabadhi ghalani, Ushirika, SIDO na sehemu nyingine, hivyo amewataka wakuu na wataalam hao kuzingatia mafunzo hayo kwani ni Muhimu Kwa utendaji wenye tija kwa Taifa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akiwa kwenye piacha ya pamoja na Wakuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji baada ya ufunguzi wa kikao hicho.
Aidha, Dkt. Musa ameelekeza katika kikao hicho cha kutoa mafunzo kwa wakuu na wataalamu hao kuwapa elimu mahususi ya uelewa zaidi kwenye matumizi ya teknolojia hasa katika matumizi ya tarakilishi (computer), Vishkwambi (tablets) na simu janja (Smartphone) sehemu hizo na kuwa na wigo mpana wa utekelezaji wa majukumu ya vitengo hivyo.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe akiwa kwenye kikao cha wataalam wa idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ngazi ya Mkoa.
Hapo awali Katibu Tawala msaidizi sehemu ya viwanda, biashara na uwekezaji Bi. Beatrice Njawa wakati akimkaribisha mgeni rasmi Dkt. Mussa amesema kikao hicho kinalenga kuwapitisha wataalam hao kwenye majukumu ya Msingi ya sehemu hiyo ili kuwajengea uwezo wa kufanya majukumu yao kwa ufanisi.
Katibu Tawala msaidizi sehemu ya viwanda, biashara na uwekezaji Bi. Beatrice Njawa akibainisha lengo la kikao kazi hicho cha wataalam wa idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Katika hatua nyingine Bi. Beatrice Njawa amemshukuru Katibu Tawala huyo Dkt. Mussa Ali Mussa kwa kukubali kuungana nao katika kikao hicho.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.