Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kuwa na ushirikiano baina ya Wahe. Madiwani, Waatendaji na wananchi ili kuiletea maendeleo Halmashauri hiyo.
Bi. Mariam ametoa rai hiyo Juni, 12, mwaka huu katika kikao maalum cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo wakati wa kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG kilichofanyika Mlimba katika tarafa ya Mngeta Wilayani Kilombero.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Mariam amesema ili kupiga hatua ya kimaendeleo kwa Halmashauri yeyote nchini ni budi kuwe na muunganiko wa pande hizo tatu na kama badala ya kuwa na misuguano ya mara kwa mara hivyo kuzorotehsha maendeleo.
“Muunganiko wa madiwani, watendaji na wananchi ndio njia bora ya kuleta maendeleo ya halmashuri ama wilaya husika, hivyo naomba muache maneno chapeni kazi ili mradi kila mmoja amuheshimu mwenzie amesema Bi. Mariam.
Aidha, amesema Halmashauri hiyo imekuwa mfano katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na inafanya vizuri katika mkoa wa Morogoro lakini ametahadharisha kuvunja makundi yaliyopo na kuimarisha ushirikiano baina ya pande hizo tatu ili Halmashauri hiyo iweza kuongeza zaidi ukusanyaji wa kimapato.
Katika hatua nyingine Katibu tawala huyo amewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea mapato ya zao la mpunga pekee huku akishauri kujikita katika kilimo cha zao la kakao kutokana na zao hilo kustawi vizuri katika maeneo mengi ya Halmashauri hiyo, kuwa na soko la uhakika na kakao yenye ubora zaidi.
Awali akitoa taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Morogoro Ndg. Mwabwanga Peter ameeleza namna kakao ya Mlimba ilivyotambulika nchi za ulaya kutokana na ubora wake hivyo ametoa wito kwa madiwani kuwahamasisha wananchi kulima kwa wingi kutokana na upatikanaji wa soko hilo.
“Wakati nikiwa Ulaya nilipewa kakao ya kutoka hapa nyumbani na niliposoma kifungashio kiliandikwa imetoka Mbingu Mkoani Morogoro nikashangaa maana ni tamu sana na hata wao wanaipenda sana ”amesema Mwabwanga.
Kwa upande wa hoja za ukaguzi, Mwabwanga ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kujibu vizuri hoja za CAG katika kipindi cha mwaka 2018 – 2019 ambapo hoja 19 kati ya 18 zilijibiwa kwa wakati na kubaki hoja moja ambayo ilitakiwa tamko la viongozi wa Mkoa huku kwa kipindi cha mwaka 2019 - 2020 hoja zilikuwa 24 kati ya hizo hoja 13.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Mhandisi Stephano Kaliwa amesema Halmashauri hiyo imepata hati inayoridhisha kwa miaka mitano mfululizo na kwa sasa wamebakiwa na hoja 10 ambazo zipo katika hatua ya utekelezaji.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.