Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amemuagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Barabara ya zege ya Kinole - Tegetero - Lubwe kutoka kampuni ya (MacDavid Company limited) kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara hiyo baada ya miezi miwili ili kusaidia Wananchi wa maeneo husika kusafirisha mazao yao kutoka mashambani ili kuongeza kipato kwa wananchi wa eneo hilo.
Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa agizo hilo Juni 11, 2024 wakati wa ziara yake kukagua miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara hiyo ya zege katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ikiwa ni mwazo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mkoani humo.
"... sisi tunachukua hiyo miezi miwili kazi iwe imekamilika sasa nyie watu wawili mtoa kazi na mpewa kazi mkakae na mkajipange kuhakikisha huo muda kazi inakamilika.." amesema Dkt. mussa
Hata hivyo Dkt. Mussa amemuagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara hiyo kusogeza karibu vifaa vya ujenzi katika eneo la kazi ili kurahisisha upatikanaji wa haraka na kazi kwenda kwa kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake Bw. Enock Waitara Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro akisoma taarifa ya mradi amesema mradi huo wa barabara una urefu wa kilomita 1.0, unagharimu shilingi milioni mia 5.8 na ujenzi umefikia asilimia 25 huku ujenzi unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 2 mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa amesema kabla ya ujenzi wa barabara hiyo wananchi walikuwa wanapata shida katika kusafirisha mazao yao hivyo ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo itaenda kupunguza adha ya usafirishaji katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine wananchi hawakuwa mbali kuishukuru Serikali yao kwa kuwaletea ujenzi wa barabara hiyo ya zege, akiwawakilisha wananchi wa maeneo hayo Bw. Rajabu Zahoro ameeleza changamoto zilizokuwepo mwazo kabla ya kuanza ujenzi huo kuwa baadhi ya magari yalikuwa yanadondoka kwa kufeli kupanda mlima hivyo ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha zege itaenda kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara kusafirisha mazao yao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.