Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka watendaji na wasimamizi wa mradi wa usambazaji endelevu wa maji Vijijini na usafi wa mazingira wa ngazi zote za Halmashauri hadi za vijiji kukamilisha ujenzi ifikapo Oktoba, Mwaka huu.
Dkt. Mussa amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya ubaguzi wa mradi wa usambazaji endelevu wa maji Vijijini na usafi wa mazingira (SRWSS) katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ikiwa na lengo la kuinua kiwango cha usafi wa mazingira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na jamii kwa ujumla.
Akifafanua zaidi, Katibu Tawala huyo wa Mkoa amesema mradi wa SRWSS unahusisha ujenzi wa vichomea taka, eneo la kunawia mikono pamoja na matundu ya vyoo kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa katika hali ya usafi kwenye vituo vya afya na zahanati, hivyo amewataka kukamilisha mradi huo mapema mwa mwezi oktoba mwaka huu.
"... mwezi wa kumi huo mliosema nisije nikasikia mara fedha zimetuishia, nataka miradi iishe mwanzoni wa oktoba..." amesema Dkt. Mussa Ali Mussa
Katibu Tawala huyo amesema vituo vingi vya zamani vimekuwa chakavu kutokana na kutokarabatiwa kwa sababu ya kusubiri fedha za Serikali kuu wakati fedha zinazopatikana katika vituo hivyo zinaweza kukarabati kwa kupaka rangi, kuweka sakafu na kubadilisha paa ili kuwa na mazingira bora.
Kwa sababu hiyo Dkt. Mussa amewataka madaktari kujirekebisha na kuwa na maeneo nadhifu pamoja na usafi binafsi kwa 99% kutokana na kazi zao za kuhudumia wagonjwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mussa Ali ameipongeza Kamati ya Kituo cha Afya cha Mlali ambao ndio wasimamizi wa mradi wa SRWSS kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na Serikali.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Dkt. Philipina Titus amesema kumekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kimfumo hususan mfumo wa NeST unaohusika na manunuzi ambao mwanzo hawakupata mafunzo, mvua za El nino na ugonjwa wa kipindupindu ambazo zimesababisha mradi huo kuchelewa katika vituo vya afya na zahanati.
Naye, Afisa Afya wa Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Laurent Gallet amewasisitiza wasimamizi wa miradi hiyo kuitumia kwa kuitunza sambamba na kutunza nyaraka muhimu zikiwemo ramani na cheti cha ukamilishwaji wa mradi kwa ajili ya matumizi mengine.
Mradi wa SRWSS ulianza mwaka wa fedha wa 2022/2023 na kutekelezwa 2023/2024 katika Halmashauri zote za Mkoa huo ili kuwa na mazingira safi na salama tayari kwa kuhudumia wagonjwa.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.