Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka watendaji na wasimamizi wa mradi wa usambazaji endelevu wa maji Vijijini na usafi wa mazingira wa ngazi zote za Halmashauri hadi za vijiji kukamilisha ujenzi ifikapo Novemba 30, Mwaka huu.
Dkt. Mussa amesema hayo Oktoba 24, Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa mradi wa usambazaji endelevu wa maji Vijijini na usafi wa mazingira (SRWSS) katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ikiwa na lengo la kuinua kiwango cha usafi wa mazingira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na jamii kwa ujumla.
Akifafanua zaidi, Katibu Tawala huyo wa Mkoa amesema mradi wa SRWSS unahusisha ujenzi wa vichomea taka, eneo la kunawia mikono pamoja na matundu ya vyoo kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa katika hali ya usafi kwenye vituo vya afya na zahanati, hivyo amewataka kukamilisha mradi huo mwezi Novemba 30, mwaka huu.
"... Mwezi Novemba huo mliosema ninyi wenyewe nisije nikasikia mara fedha zimetuishia, nataka miradi iishe hiyo Novemba Mwaka huu..." amesema Dkt. Mussa Ali Mussa
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Laurent Gallet amewasisitiza wasimamizi wa miradi hiyo kuwajibika ipasavyo bila kuwa na visingizio vya mfumo wa NeST na kusisitiza ushirikiano katika idara zote zinazohusika ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Malinyi Bw. Khamis Katimba amesema kumekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kimfumo hususan mwitikio mdogo wa wasambazaji wa vifaa (wazabuni) katika Halmashauri hiyo hivyo wamefanya juhudi za kuwatafuta wazabuni hao ili kuanza ujenzi huo na kukamilika kwa wakati.
Mradi wa SRWSS ulianza mwaka wa fedha wa 2022/2023 na kutekelezwa 2023/2024 katika Halmashauri zote za Mkoa huo ili kuwa na mazingira safi na salama tayari kwa kuhudumia wagonjwa.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.