Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameupongeza Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki – EAMCEF, kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuwapatia wananchi waishio karibu na maeneo ya hifadhi hiyo njia mbadala ya kujipatia kipato.
Dkt. Mussa ametoa pongezi hizo Machi 2, 2024 wakati wa ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo yanayonufaika na ikiwemo kata ya Luhungo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Baada ya kuwatembelea wanufaika wa ufadhili wa mfuko wa EAMCEF wa kata hiyo ya Luhungo, Dkt. Mussa Ali Mussa amebainisha mbele ya wananchi wa kata hiyo wanaonufaika na maradi huo kuwa lengo mahususi ni kupunguza umaskini miongoni mwao ili kuondoa uharibifu wa misitu hiyo. Miongoni mwa miradi iliyofadhiliwa na EAMCEF ni Pamoja na kuanzisha miradi ya kiuchumi ukiwemo ufugaji wa mbuzi wa maziwa, mradi wa uzalishaji uyoga na mradi wa matumizi ya majiko banifu.
Katibu Tawala huyo amesema miradi mingine ni mradi wa kilimo cha mazao ya viungo kama karafuu, Mdarasini, vanilla mchaichai na mbogamboga huku akiwataka wananchi wa maeneo ya hifadhi hiyo kuimarisha zaidi miradi hiyo ili kujipatia kipato na hatimae kupunguza uharibifu wa misitu.
“...ombi langu tufuge mbuzi kwa wingi, tuzalishe huo uyoga kwa wingi, ombi langu tupande michaichai kwa wingi, ombi langu tupande mikarafuu kwa wingi....” amesema Dkt. Mussa
Naye Afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Bw. Joseph Chuwa amesema Milima ya Tao la Mashariki ni safu za milima imepita katika mikoa Minne ya Morogoro, Kilimanjaro, Tanga na Iringa huku akibainisha kuwa miradi inayotekelezwa na Mfuko wa EAMCEF kwa Mkoa wa Morogoro unatekelezwa katika Halmashauri za tano za Mkoa huo ikiwemo Morogoro Manispaa, Mvomero, Halmashsuri ya Mji Ifakara, Mlimba na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Bw. Chuwa ameongeza kuwa mito mikubwa ikiwemo mto Ruvu, Zigi, Wami, Ruaha na mto Pangani ambayo hutiririsha maji yao katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es Salaam huhu zaidi ya asilimia 25 ya wananchi wanaoishi karibu na milima ya Tao la mashariki wanategemea maji hayo kwa shughuli za mashambani na matumizi mengine.
Pia amesema, milima hiyo inachangia katika uzalishaji wa umeme ambapo kwa zaidi ya asilimia 50 ya umeme wote unaosambazwa hapa nchini Tanzania unatokana na maji huku akieleza kuwa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Mwalimu Nyerere yote yanategemea maji kutoka misitu ya milima hii ya Tao la Mashariki
Kwa upande wao wanufaika wa miradi hiyo akiwemo Bi. Hanifa Salumu Mkazi wa Luhungo amewashukuru wafadhili wa mradi huo huku akibainisha kuwa alianza kufuga mbuzi wa maziwa mmoja hadi sasa ana mbuzi wanne hivyo mradi huo utamsaidia kupata kipato na kuacha kuharibu misitu iliyopo katika misitu ya milima hiyo kwa sababu ya kutafuta kuni.
Tao la Mashariki ni safu ya Milima iliyofunikwa na misitu yenye unyevu pamoja na mbuga katika nchi ya Tanzania na Kenya. Milima hiyo ina sifa ya kuhifadhi vyanzo vya maji ambayo hutumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo matumizi ya majumbani, uzalishaji wa umeme na shughuli za kilimo.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.