RAS morogoro awafunda watumishi wa umma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja ametoa wito kwa Watumishi wa Umma Mkoani humo kujishughulisha na kilimo na Biashara ili kuboresha maisha yao na familia zao badala ya kutegemea mishahara ya kazi zao pekee.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro (RAS) Bi. Mariam Mtunguja wakati wa kikao cha kusikiliza na kupokea changamoto za watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Juni, 23 mwaka huu.
Bi. Mariam ametoa wito huo Juni 23 mwaka huu wakati wa kikao na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alichokiitisha ili kufahamiana zaidi pamoja na kusikiliza kero walizo nazo watumishi hao kikao ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utumishi na Utawala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bw. Herman P. Tesha akisikiliza kwa makini maelekezo wakati wa kikao hicho.
RAS (aliyejivika kitambaa cheupe kichwani) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi yake mara baada ya kikao hicho. Ni picha inayoonesha kikao kimeamsha ari ya kazi kwa watumishi hao. Kazi iendelee.
Bi. Mtunguja amesema, kipato kinachotokana na mishahara yao pekee hakitasaidia kuboresha maisha yao kama watumishi hao hawatakuwa na njia nyingine ya kujikimu huku akiwashauri kujikita kwenye kilimo na biashara kazi ambazo amesema wanaweza kuzifanya baada ya masaa ya kazi za Ofisi.
“sisi tujishughulishe na kilimo, tujishughulishe na biashara na kwa bahati nzuri Mkoa wetu uko vizuri” amesema Mariam Mtunguja.
Watumishi wakionekana wana hamu ya kuendelea kusikia maneno yenye faraja kutoka kwa kiongozi wao - RAS
Pamoja na kuwahamasisha watumishi hao kujikita katika kilimo na biashara amewatahadharisha wastaafu au watumishi wanakaribia kustaafu kutojiingiza kwenye biashara wasizozifahamu vema kwa kuwa wanaweza kutapeliwa kirahisi na kupoteza fedha zao.
“Msije mkajiingiza kwenye biashara ambazo hamzijui, ukiwa mstaafu usije ukajiingiza kwenye biashara usioijua watakuumiza, watu wamepigwa sana, afadhari hata kwenye kilimo..” amesisitiza Bi. Mtunguja.
kwa upande wao watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo akiwemo Leocardia Ramadhani na Pendo Daniel walieleza namna walivyompokea Katibu Tawala huyo na kubainisha kuwa amewatia moyo kwa kupokea changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi.
Aidha, wamempongeza kwa kuwajengea mazingira rafiki ya kuunda vikundi vya kusaidiana katika masuala ya kijamii yatakayosaidia kuondoa mifadhaiko wakiwa kazini na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Eric Olomi (Mchumi) kutoka Idara ya Mipango na Uratibu, akionekana kumkubali Boss wake Bi. Mariam Mtunguja kwa kile kinachotolewa nae wakati wa kikao hicho.
Naye Alhaji Hamisi Sengulo ambaye pia ni mtumishi katika Ofisi hiyo, yeye amekwenda mbali zaidi kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuteua Viongozi mahiri wa kumsaidia katika kazi ya kuwatumikia watanzania huku akiwataja Mkuu wa Mkoa wa Morogorogo Martine Shigela na Katibu Tawala wake Mariam Mtunguja kuwa kwa muda mfupi waliokaa, tayari wametoa maamuzi kadhaa ambayo yote yamelenga kupunguza kero za wananchi na kuwaletea maendeleo ya kweli.
Alhaji Hamis Sengulo akiwa katika kikao cha Katibu Tawala wa Mkoa huku akisikiliza kwa makini maelekezo yanayotolewa
watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakiwa katika kikao hicho, hapa wakitoa maoni, changamoto pamoja na mapendekezo yao kwa mtindo wa kuandika kwenye karatasi.
nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...KAZI IENDELEE
Imeandaliwa na Afisa Habari na Mahusiano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
(Picha zote na Andrew Tangazo Chimesela)
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.