Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wametakiwa kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi huku akiwataka kutumia vema mazingira mazuri ya Ofisi hiyo katika kufanya mazoezi kwa lengo la kuiweka timamu miili yao na kuepusha magonjwa madogomadogo yanayoweza kuepukika.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 3, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa wakati akizindua rasmi klabu ya mazoezi ya Ofisi hiyo iliyofanyika eneo la maporomoko ya Maji ya CHOMA yaliyopo nje kidogo na Ofisi hiyo.
Amesema, Ofisi yake imefikia uamuzi wa kuanzisha “Club” hiyo inayojulikana kwa jina la “RAS MOROGORO JOGGING CLUB” ili kuimarisha Afya za watumishi wake na kutekeleza agizo la Serikali la kila Ofisi ya Umma iwe na program ya watumishi wake kufanya mazoezi ili kulinda afya za watumishi hao.
Aidha, amesema mazoezi hayo yatakuwa endelevu huku akibainisha kuwa yatakwenda sambamba na kutembelea maeneo ya utalii kama walivyotembelea maporomoko ya CHOMA ili kuyatangaza lakini pia kuyaboresha pale inapobidi kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika.
Amesema, Ofisi yake itakuwa tayari kushirikiana na Viongozi wa Sekta mbalimbali na kupeleka mahitaji muhimu kama UMeme, Maji, Barabara na huduma za Afya ili kuhakikisha Maisha ya wanaozunguka vivutio hivyo yanaboreka na kunyanyua Maisha yao Pamoja na kuongeza thamani ya maeneo hayo.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo amesema kuzinduliwa kwa klabu hiyo kunachocheo maandalizi ya kwenda kupata ushindi wa kishindo kwenye mashindano ya shirikisho la michezo ya wizara na idara za serikali (SHIMIWI) yanayotarajiwa kufanyika Jijini Mwanza kuanzia Septemba 1 hadi 16 mwaka huu.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Michezo Mkoa wa Morogoro Grace Njau amesema ili mazoezi ya watumishi kuwa endelevu imewekwa ratiba maalum ya siku tatu kwa wiki kuanzia saa 10:00 hadi saa 11:00 jioni watumishi wote wanaungana Pamoja kufanya mazoezi.
Naye Bw. Justine Mnyandwa kwa niaba ya watumishi wa Ofisi hiyo amesema kuwa kuna faida kubwa ya kufanya mazoezi hayo, amesema nje ya kuimarisha Afya za watumishi kwa kuepuka magonjwa yasiyoambukiza bado mazoezi hayo yanadumisha Ushirikiano, Upendo na umoja miongoni mwa watumishi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.