Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amewataka Watanzania kutumia maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) katika kanda zao kwa ajili ya kupata Elimu mpya ya kufanya shughuli zao za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na tija zaidi na kuinua uchumi wao na wa Taifa.
Mhe. Chalamila ametoa kauli hiyo Agosti 5, mwaka huu wakati akitembelea mabanda ya bidhaa na vipando kwenye maonesho ya 32 ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema, katika sekta ya kilimo, Serikali inaendelea kutenga bajeti kubwa ya fedha ili kuhakikisha kilimo kinakuwa sekta inayochangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya taifa, ambapo wakulima wameendelea kupata mbolea na vifaa vya kisasa vya kilimo kuliko miaka ya nyuma.
“Nitoe rai kwa Watanzania wote kutumia maonesho haya ya Nanenane katika kanda zenu ili muweze kupata maarifa mapya,” amesema Mhe. Albert Chalamila.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alipotembelea banda la Wakala wa Vipimo Tanzania amesisitiza umuhimu wa kutumia vipimo sahihi vilivyokubaliwa na mamlaka husika na wanaokiuka taratibu kwa kutumia mizani au vipimo vingine visivyothibitishwa na Mamlaka na kuwaibia wakulima watachukuliwa hatua za kisheria wakiwemo wanaojihusisha na vipimo vya lumbesa.
Katika hatua nyingine Mhe. Chalamila amewapongeza wadau mbalimbali waliojitokeza kushiriki maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki na kubainisha kuwa yamekuwa na upekee kwa kuwa kumekuwa na bidhaa nyingi mna bora huku akiwataka wananchi kufika kwa wingi katika maonesho hayo ili kupata ujuzi na mbinu mpya za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.