Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro (RAS) Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kupeleka fedha kwenye vitengo vya Ukaguzi wa ndani Ili vitengo hivyo viweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe Dunstan Kyobya (wa tatu kulia waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa na Halmashauri pamoja na Wataalam wa idara ya Ukaguzi wa Ndani, wengine ni Katibu Tawala Wilaya ya Kilombero Bw. Abraham Mwaikwila, Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi Bi. Neema Dachi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Morogoro CPA Peter Mwabwanga.
Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa agizo hilo Septemba 5, 2023 wakati wa kufungua kikao kazi cha kawaida cha wakaguzi wa ndani Mkoani humo kilichofanyika Katika Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero, amesema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Dunstan Kyobya.
CPA Peter Mwabwanga akielekeza Jambo wakati wa kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi Bi. Neema Dachi.
Akisoma hotuba hiyo kwa niaba ya RAS, Mhe. Dustan kyobya amesema wakaguzi wa ndani katika Halmashauri wanazo changamoto nyingi, mojawapo na ufinyu wa bajeti, hata hivyo amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa huo kupeleka fedha kwenye vitengo hivyo kulingana na bajeti ya Halmashauri iliyopitishwa.
"...naomba kutoa rai kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kuhakikisha; moja mnapeleka fedha Katika Vitengo vya Ukaguzi wa ndani kwa mujibu wa bajeti ya Halmashauri iliyopitishwa" amesema Dkt. Mussa Ali Mussa.
Aidha, amesema kwa kuwa Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto za Kitengo hicho ikiwemo idadi ya watumishi isiyo timilifu, uhaba wa vitendea kazi na ufinyu wa bajeti, bado amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vitengo hivyo hususan kuwawezesha usafiri pale wanapohitaji kwenda kutekeleza majukumu yao ya kiofisi.
Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi Bi. Neema Dachi akiwa kwenye kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani.
Katika hatua nyingine Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka Wakaguzi wa ndani kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia miiko ya kazi zao lakini pia wajiamini huku akiwataka kutokuwa na kigugumizi cha kuwachukulia hatua za kisheria watumishi watakaobainika kufanya ubadhilifu wa fedha za Umma.
Sambamba na hayo amewataka kupunguza hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazotokea Katika Halmashauri zao, kufanya ukaguzi wa ndani kila robo mwaka, kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Halmashauri zao, kufanya kazi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano - TEHAMA pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya na Viongozi wengine wa ngazi ya Wilaya na Mkoa.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kilikuwa na lengo la kukumbushana wajibu na majukumu ya Wakaguzi wa ndani huku Katibu Tawala wa Mkoa akitoa wito kwa wakaguzi wa ndani kufika Katika Ofisi yake mara wanapokuwa na changamoto zote.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.