Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka Vijana Mkoani humo kuchangamkia fursa zinazopatikana katika Mkoa huo hususan za uongezaji wa thamani kwenye mazao ya kilimo yakiwemo mazao ya Viungo, Matunda na mbogamboga kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
Dkt. Mussa ametoa wito huo Februari 16, 2024 wakati akifunga mafunzo ya usindikaji wa mazao ya viungo, matunda na mbogamboga katika ofisi za shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo - SIDO Mkoani Morogoro.
Katibu Tawala huyo amesema kuwa Serikali ya Mkoa huo imejitahidi kuweka fursa mbalimbali kwenye kilimo kwa kuamua kulima mazao ya biashara pamoja na mazao ya viungo ambayo yatawasaidia wananchi Mkoani humo kukuza uchumi wao, hivyo amesisitiza wananchi hususan vijana kujikita katika kutumia fursa ambazo zimeletwa na Serikali yao.
“.. nyinyi wenyewe muwe tayari kuthamini hizo juhudi tulizozichukua na mkubali kujiondoa sehemu mliyopo ili mfike hatua nyingine...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa amesema Mkoa huo utaendelea kuweka mazingira bora kwa Vjiana ili waweze kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na utoaji wa mikopo ya asilimia 10. Hata hivyo, amesema changamoto zilizotajwa na wahitimu hao Serikali imezichukua ili kuangalia namna ya kuzitatua.
Naye Meneja wa SIDO Mkoa wa Morogoro Bi. Joan Nangawe amesema shirika hilo linawasaidia wajasiliamali katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ya Teknolojia kwa kuwapatia mashine kwa ajili ya kuendesha biashara zao pia wanatoa mafunzo ya usindikaji na uongezaji wa thamani kwenye mazao ya viungo, matunda na mbogamboga, mafunzo ya ususi na ushonaji huku akibainisha kuwa wameweza kuwafikia wajasiriamali 400 lengo ni kuwafikia wajasiriamali 1000 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.
Ameongeza kuwa shirika linawasaidia wajasiriamali kupata nembo za ubora kutoka shirika la viwango nchini (TBS) pamoja na kuwapatia mikopo ambapo hadi sasa wamekopeshwa wajasiriamali 71 ambao wamechukua jumla ya shilingi 300,000,000/=.
Kwa upande wao wahitimu wa Mafunzo hayo akiwemo Bw. Mosses Joseph amesema mafunzo hayo yalikuwa kwa kipindi cha wiki moja ambayo yalianza Februari 12 - 16, 2024 wakiwa jumla ya wanafunzi 33 kati yao wanawake ni 22 na wanaume 11.
Bw. Mosses ameeleza changamoto zinazowakabili hususan kwenye uzalishaji ikiwa ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi, kutokuwa na mtaji wa kutosha hali inayowafanya kushindwa kuzalisha kwa wingi bidhaa zao na kukosekana kwa masoko ya uhakika.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.