Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akizungumza na wadau wa Lishe waliohudhuria kikao hicho.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Musa Ali Musa amewataka watendaji wa Serikali Mkoani Morogoro hususan maafisa lishe kujitathmini kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Lishe na kuhakikisha wanautekeleza Mkataba huo kwa mujibu wa Mkataba pasi na kukwepesha fedha zinazotolewa kwa ajili hiyo.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Bw. Herman Tesha (kulia), Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Kusirye Ukio (katikati) pamoja na Bw. Steven Benedict Mkaguzi wa Ndani Mkoani Morogoro wakati wa kikao cha tathmini ya Mkataba wa lishe.
Dkt. Mussa Ali Mussa amesema hayo juni 2, 2023 wakati wa kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe ngazi ya Mkoa kwa kipindi cha januari - machi mwaka huu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
"Kwa hiyo sisi wenyewe tuanze kujitathmini...kila anayejiona amewekewa alama nyekundu, njano au nyeupe muanze kuchukua hatua kama hii niliyochukua mimi..." Amesema.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye kikao.
Dkt. Musa amebainisha kuwa Mkoa huo haufanyi vizuri suala la lishe kutokana na baadhi ya watendaji ngazi ya Wilaya kutokuwa na umakini katika kutekeleza mkataba huo na kuwataka viongozi wao kupambana na uzembe unaojitokeza kwani Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anadhamira ya dhati na Afya za watoto na kwa jamii nzima kwa ujumla.
Sambamba na maagizo hayo, amewashauri watendaji hao kujikita katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora ili kuondokana tatizo la udumavu wa akili na mwili, kwani madhara ya kukosa lishe bora hupelekea kudumaa, Ngozi kusinyaa, utapiamlo, kwashakoo na matatizo mengine mengi.
Kwa upande wake, Afisa lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amewaomba watendaji ngazi ya jamii ambao nao walisaini mkataba wa lishe wanatakiwa kushirikiana vema na halmashauri kupeleka huduma za chakula mashuleni kwa kuzingatia watoto wote badala ya kutoa chakula hicho kwa madarasa machache.
Afisa Lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe akiwasilisha hali ya lishe ya Mkoa huo.
Aidha, amesisitiza kutoa Elimu ya lishe kwa wazazi au walezi na ndugu kushirikiana na serikali katika kutoa chakula kwa watoto mashuleni kwani chakula kinachotumika shuleni kwa mtoto ni kile kile ambacho kingetumika kwa mtoto huyo wakati akiwa nyumbani.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira (kushoto) akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro Mhe. Rehema Bwasi wakati wa kikao.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.