Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka waalimu wa Shule za Sekondari na Msingi Mkoani humo kuwa wabunifu katika kuwapatia wanafunzi vyakula vya asili mashuleni ili wanafunzi hao waweze kujenga utimamu wa kimwili na kiakili kutokana na lishe inayopatikana kwenye vyakula hivyo.
Dkt. Mussa Ali Mussa amesema hayo Agosti 26, 2024 akiwa katika shule ya msingi Bamba iliyopo Kata ya Kiroka katika ziara yake yenye lengo la kutembelea shule mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kukagua vyakula vinavyoliwa mashuleni na wanafunzi ndani ya Halmashauri hiyo
Dkt Mussa amesema vyakula vya asili vinavyopatikana kwenye maeneo mengi ya Mkoa huo yakiwemo Mashelisheli, viazi, mihogo na ndizi vina lishe muhimu kwa watu wote hivyo vinapaswa kupikwa kwa namna tofauti ili kuwavutia wanafunzi kwa kuwa ndio vyakula vyao vya kila siku hivyo bila kuwaandalia vizuri hawatavutiwa na vyakula hivyo.
“… kuna vitu naomba mbadilike, kupunguza mzigo kwa wazazi ili hawa Watoto wote wapate kula, hilo tatizo limekuwepo ni kwa sababu walimu hamjataka kubadilika…” amesema Dkt. Mussa Aili Mussa
Aidha, Katibu Tawala huyo amesema vyakula hivyo vinapunguza gharama kwa wazazi kununua vyakula na kutoa fedha za ada ya wapishi ambapo hujikuta wazazi wachache wanachangia michango hiyo huku wengine wakitaka kutoa baadhi ya mazao ikiwa ni mbadala wa michango hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mussa amewataka walimu wa shule hizo kulima mboga mboga na mazao ya biashara kama michikichi, mashelisheli na mikarafuu na kubainisha kuwa miche ya mikarafuu 40 inaweza kuleta faida ya shilingi 9 mil. ndani ya miaka minne hivyo shule husika kuweza kujiendesha yenyewe.
Kwa upande wake, Afisa lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amesema, vyakula vingi hususan vya mashuleni wanafunzi hawapati mlo kamili na kusababisha watoto kusumbuliwa na magonjwa.
Kwa sababu hiyo Bi Salome amewasisitiza walimu kutumia mboga za majani za asili kwa wingi zikiwemo mchunga, mchicha pori, mnafu na majani ya kunde lengo ni kujenga afya ya watoto kwani mboga hizo hupatikana kwa urahisi.
Pia amesema walimu wanatakiwa kutumia matunda yaliyopo katika maeneo yao hususan maembe, machungwa na parachichi wakati wote wa chakula ili kutoa mlo kamili wenye lishe ya kutosheleza kwa Wanafunzi.
Naye, Mwalimu anayehusika na kuratibu upatikanaji wa chakula cha Shule ya Msingi ya Mtongozi Bw. Benard Swai amethibitisha kuwa katika shule hiyo wanafunzi wanatumia matunda ya mishelisheli na mboga mboga lengo ni kuweza wanafunzi kuhimili darasani kwa kusikiliza na kuelewa kinachofundishwa.
Mwisho.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.