Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka wananchi wilayani Kilosa kutunza miundombinu ya barabara, madaraja na mitaro ya kupitishia maji ili iweze kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt. Mussa ametoa wito huo Juni 13, 2024 wakati akikagua miundombinu ya madaraja ya Mazinyungu, Ilonga na Kobe yaliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu ya kukagua miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara.
Dkt. Mussa amesema kuna umuhimu mkubwa wa wananchi wa maeneo hayo kutunza miundombinu hiyo ikiwemo kusafisha mitaro ya maji pindi inapochafuka ili kuepusha maji kutoka nje ya mitaro na kusababisha maafa kwa wananchi, huku akiwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu ya barabara hususan alama za barabarani.
"...ombi letu ni lilelile ili miundombinu hii ilete faida lazima itunzwe na isafishwe ikisafishwa inamaana itadumu..." amesema Dkt. Mussa
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu yakiwemo madaraja ni Bilioni 36 na zimefanikisha kukamilisha ujenzi wa madaraja matatu ambayo ni daraja la Mazinyungu, daraja la Kobe na Ilonga pia kupitia fedha za dharura zimesaidia kukamilisha ujenzi wa mitaro ya maji na kwenda kupunguza adha ya mafuriko Wilayani humo.
Aidha, Mhe. Shaka ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali wananchi wa Kilosa kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madaraja na mitaro ya maji ambapo hapo awali walikuwa wanapata changamoto ya mafuriko kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu hiyo.
Naye Diwani wa Kata ya Mvumi Ndg. Shabani Mabingo amesema kupitia ujenzi wa miundombinu hususan mitaro umeenda kuondoa adha ya mafuriko katika kata hiyo hivyo amemhakikishia Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro kuitunza kwa kushirikiana na wananchi ili iweze kuwa safi pindi mvua zinaponyesha maji yake yaweze kupita bila changamoto.
Nao wananchi wa Kilosa akiwemo Alfonce Dimoso mkazi wa Kijiji cha Mazese B wameishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa madaraja hayo ambapo imeenda kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo yao.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kilosa Mjini Irene Vedastus amesema hapo awali walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda shule kutokana na kutopitika kwa daraja la Mazinyungu hivyo kukamilika kwa daraja hilo kumewapunguzia umbali na kufika shuleni kwa wakati.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.