RAS Morogoro azindua kampeni kuhamasisha utoaji chakula shuleni kwa kutumia vyakula vya asili.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amezindua kampeni ya kuhamasisha utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Mkoani Morogoro kwa kutumia vyakula vya asili vinavyopatikana Mkoani humo.
Dkt. Mussa Ali Mussa amezindua kampeni hiyo Januari 19, 2024 katika viwanja vya shule ya msingi Mtombozi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa lengo la kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi Mkoani.
Dkt. Mussa mesema, Mkoa huo umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za vyakula vya asili vikiwemo mashelisheli, mihogo, Viazi vitamu na ndizi huku akisema kuwa haoni sababu ya wanafunzi kukosa chakula cha mchana na kuwataka wazazi kwa kushirikiana na Walimu kufanikisha upatikanaji wa vyakula hivyo kulingana na maeneo husika.
“...kuja kwangu leo hapa ni kuanzisha hii kampeni, si kwa hapa tu lakini kwa Halmashauri nzima na Morogoro nzima lazima tukubali kutumia vyakula vyetu vya asili tulivyokuwa navyo...” amesema Dkt. Mussa.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameongoza Viongozi, wazazi na wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kupata chakula cha asili mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni kwa kutumia vyakula vya asili.
Aidha, Katibu Tawala huyo ameeleza kuwa kukosekana kwa chakula cha mchana kuna sababisha utoro na kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi. Pamoja na uzinduzi wa kampeni hiyo ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuhakikisha kuwa inapanda miche ya mashelisheli angalau miche miwili kwa kila shule zote Wilayani humo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akipokea zawadi ya vyakula vya asili vikiwemo Mashelisheli, Ndizi, Magimbi na Mihogo kutoka kwa Diwani Kata ya Mtombozi Mhe. Yahaya Mfaume kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo.
Naye Afisa Lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amewashauri wazazi na walezi kuzingatia makundi matano ya vyakula Vikiwemo vyakula vya protini, wanga, Vitamini, mafuta na mboga mboga ili kupata mlo kamili kwa ajili ya kuboresha afya za watoto wao.
Afisa lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe akifafanua kuhusu umuhimu wa lishe kwa kuzingatia makundi matano ya chakula wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni kwa kutumia vyakula vya asili.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro amemshukuru Katibu Tawala huyo kwa kuzindua kampeni hiyo ambayo itasaidia kupandisha kiwango cha ufaulu katika Halmashauri na kumhakikishia kuwa watatekeleza maagizo aliyoyatoa.
Katika kuhamasisha kampeni hiyo Dkt. Mussa ameahidi kuichangia shule ya msingi Mtombozi dagaa kilo 100 kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Mkoa huo kuchukua taadhali ya ugonjwa wa kipindupindu ambao umekuwa tishio hapa nchini.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.