Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amekemea vikali baadhi ya mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani humo kuwa na tabia ya kutafuta maslahi binafsi badala ya mashirika hayo kuwaletea wananchi maendeleo yao.
Dkt. Musaa ametoa kauli hiyo Julai 8, 2024 wakati akifungua semina ya mafunzo ya kuyajengea uwezo mashirika yasiyo ya kiserikali iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Amesema, lengo la kuazishwa kwa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali ni kuisaidia jamii, hivyo amezitaka kila NGOs mkoani humo kutekeleza lengo la kuanzishwa kwake badala ya kujinufaisha.
Akibainisha zaidi Dkt. Mussa amesema, baadhi ya mashirika hayo yakipata fedha kutoka Serikalini huwa hawatimizi malengo waliyojiwekea ambapo ni kinyume na taratibu walizojiwekea.
"....Hizi NGOs huwa zinatumika vibaya, yale mambo wanayotakiwa wayafanye huwa hawayafanyi, hizi NGOs badaya ya kuwa msaada kwa yale makundi ambayo yamekusudiwa bali hujisaidia wao wenyewe..." amesisitiza Dkt. Mussa
Kwa sababu hiyo, Dkt. Mussa ameonya vikali kuwa NGOs yoyote Mkoani humo itakayokiuka na kwenda kinyume na malengo yake ya uazishwaji itachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufutiwa usajili wake.
Kwa upande Wake Bi. Vidah Malle kutoka Wizara ya fedha amesema mafunzo hayo yataenda kuyajengea uwezo mashirika yasio ya kiserikali katika utekelezaji wa majukumu yao, kufahamu sheria na miongozo mbalimbali, kufahamu kuandaa bajeti nzima ya serikali na mchango wao katika bajeti hiyo.
Naye kiongozi wa Baraza la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) Mkoa wa Morogoro Bw. Otanamusu Nicholaus amesema mafunzo waliyoyapata yatasaidia kuyajenga mashirika hayo katika ngazi zote Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Amesema, lengo la mashirika hayo ni kusaidia jamii hivyo ameyataka mashirika yanayopata fedha kutoka Serikalini kuacha tabia ya kutafuta maslahi binafsi badala yake fedha hizo zitumike kuiletea jamii maendeleo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.