Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameagiza shule zote za Mkoa wa Morogoro kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni jitihada za kuunga mkono na kutekeleza maagizo ya serikali ya kulinda mazingira ili kuondokana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Dkt. Mussa ametoa agizo hilo Septemba 4, mwaka huu akiwa Wilayani Gairo Mkoani humo akiendelea na ziara yake ya kuangalia hali ya lishe mashuleni na kukagua utekelezaji wa maagizo ya serikali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema, athari zinazotokana na nishati chafu ya kupikia ni pamoja na magonjwa katika mfumo wa upumuaji, mazingira hatarishi wakati wa kutafuta kuni na kuhatarisha upotevu wa misitu, hivyo amezitaka taasisi mbalimbali Mkoani humo zikiwemo shule za msingi na Sekondari kutumia nishati safi ya kupikia.
“…agizo la serikali lilishatolewa kila penye watu mia wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia mkae muwashauri walimu katika shule zao waache matumizi ya kuni…” amesema Katibu Tawala wa huyo wa Mkoa
Katika hatua nyigine, Dkt. Mussa amewataka maafisa kilimo kuanzia ngazi ya halmashauri hadi ya Kijiji kushirikiana na walimu wa shule za Msingi na Sekondari kuwapa elimu bora ya kilimo na kutoa mbegu bora, mbolea na dawa za kuua wadudu ili kulima mboga mboga, hivyo kuimarisha lishe bora kwa wanafunzi.
Afisa Lishe wa Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Richard Magoma amesema walimu pamoja na kamati ya shule inapaswa kubaini namna bora ya kuwashawishi wazazi kuchangia chakula ikiwemo kutoa chakula kinachopatikana katika maeneo wanayoishi.
Naye, Afisa elimu ya watu wazima na elimu maalum Mkoa wa Morogoro Bi. Rodha Sheba Murusuri amewashauri walimu wa shule hizo kulima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi pamoja na mbaazi ili kupunguza mzigo kwa wazazi kuchangia maharage kwa ajili ya mboga.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.