RC Morogoro aanza ziara rasmi ya kikazi na kujitambulisha
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Abourbakar Mwassa ameanza rasmi ziara ya kujitambulisha kwa wananchi wa Mkoa huo katika Halmashauri zote tisa (9) za Mkoa huo lengo likiwa ni kuutambua vema Mkoa, kutambua changamoto zinazowakabili wananchi na kutambua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa alipofika katika mradi wa kituo cha kusukuma maji cha Kihonda
Fatma Mwassa ameanza ziara hiyo leo Septemba 12 katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya ziara ya aina hiyo tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo Agosti Mosi mwaka huu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Ally Machela akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, alipotembelea miradi ya maendeleo
Akiwa katika Halmashauri hiyo Mkuu huyo wa Mkoa ametembelea miradi ya Maendeleo nane(8) ukiwemo mradi wa Shule ya Sekondari ya Boma yenye gorofa mbili Kituo cha Afya cha Tungi, Kituo cha Afya cha Lukobe, Shule ya Sekondari ya Lukobe, Hospitali ya Halamshauri ya Manispaa pamoja na Shule ya sekondari ya Mindu.
Miradi mingine aliyoitembelea ni ya Ujenzi wa Barabara ya Manzimbu inayojengwa na wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) na ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma maji eneo la Kihonda Mizani ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi 593 Mil.
Akiwa katika Mradi wa ujenzi wa Tanki la Maji Kihonda Fatma Mwassa amewataka wananchi wa Mkoa huo kutoharibu vyanzo vya maji kwa kuchungia mifugo katika maeneo hayo ya vyanzo vya maji na kutokukata miti karibu na maeneo hayo jambo ambalo amesema hatolivumilia kamwe.
Akisisitiza zaidi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji Fatma Mwassa amewataka wanasiasa wakiwemo Waheshimiwa. Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kuungana pamoja kukemea mwananchi yeyote anayeharibu vyanzo vya maji kwa kuwa maji ni uhai na kutumia fursa hiyo kuwataka waheshimiwa. Madiwani kuacha “siasa nyepesi”.
“Mimi niwaombe sana Waheshimiwa. Madiwani wangu, tusifanye siasa nyepesi nyepesi, kwenye suala la maji sheria lazima ichukue mkondo wake vinginevyo hakutakuwa na sababu ya sisi kuwepo....”amesema Fatma Mwassa
Amesema upatikanaji wa Maji kwa Manispaa ya Morogoro ni 48% lakini serikali imeelekeza upatikana wa maji Mijini ni 98%, hii haimaanishi Serikali haijafanya kazi yake kuwapelekea wananchi maji la hasha, Serikali imeweka miundombinu ya maji ya kutosha takribani kila eneo changamoto ni uhaba wa maji yenyewe kunakotokana na uharibufu wa vyanzo vya maji kunakofanywa na wananchi wachache wasioitakia mema nchi hii.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) Mhandisi Tamimu Katakwebe amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa tanki hilo la maji linalojengwa kwa shilingi 593.3 Mil. kwa fedha za Serikali amba[po kuna pampu mbili zenye uwezo wa kupandisha maji lita milioni 2 kwa saa 8 ambalo litanufaisha wakazi 120,000 wa kata za Kiegea, Mkundi na Mgulu wa Ndege.
Mkuu wa Mkoa fFatma Mwassa kesho Septemba 13 anaendelea na ziara katika Halmashauri hiyo ambapo anategemewa kuwa na Mkuatano na wananchim ili sikiliza kero zao na kuzitatua.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.