Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewataka wananchi wa Mikoa ya Tanga, Pwani, Dar Es Salaam, Morogoro na mikoa ya jirani kushiriki kikamilifu maadhimisho ya siku ya wakulima maarufu kama Nanenane kwa lengo la kujipatia maarifa na utaalam mpya wa kuendesha shughuli zinazohusu kilimo, ufugaji na Uvuvi.
Mhe. Chalamila ametoa kauli hiyo wakati akifunga kikao cha maandalizi ya sherehe za nanenane 2024 Kanda ya Mashariki kilichofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni maandalizi ya mwishoni ya maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 8 mwaka huu.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema sherehe za Nanenane za mwaka huu ni za kipekee kutokana na uwepo wa mvua za kutosha zilizowezesha kustawisha mazao ya kutosha kwa maeneo mengi hapa nchini, hivyo wananchi watapata fursa ya kuona vipando vya mazao mbalimbali, mifugo na uvuvi katika maadhimisho hayo na kujifunza teknolojia mpya katika sekta hizo.
"... Wananchi wote waamshwe na kengele ya nanenane, nanenane ya mwaka 2024 ni nanenane ya kipekee.." amesema Mhe. Chalamila.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha Sekta ya Kilimo na kuhama kutoka kilimo siasa (political Agriculture) kwenda kwenye kilimo cha kiuchumi (Economic Agriculture) kikiwa na nia ya kumsaidia mkulima kuzalisha mazao yenye viwango yanayoendana na soko la kimataifa hivyo kuboresha maisha ya mtanzania.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.