Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika Mkoa huo.
Shukrani hizo zimetolewa Disemba 21 mwaka huu alipotembelea mradi wa ujenzi wa tanki la maji lililopo eneo la Kiegea katika Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Fatma Mwassa amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani ametoa zaidi ya shilingi Bilioni 200 ambapo fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi midogo midogo ya maji ambayo itawanufaisha wakazi zaidi ya 120,000 wa Kihegea, Kihonda na Star City nashilingi Bilioni 185 kwa ajili ya uboreshaji wa bwawa la Mindu na ujenzi wa kituo cha kutibu maji katika eneo la Mafiga katika Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesema Mkoa wa Morogoro unakabiliwa na kero kubwa tatu ambazo ni upatikanaji wa maji, migogoro ya ardhi pamoja na miundombinu ya barabara hivyo Serikali imeweka juhudi kubwa katika kukabiliana na kero hizo ili kuzipunguza na kama ikiwezekana kuzimaliza kabisa.
Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amewataka wananchi katika Mkoa huo kutii sheria na kutii taratibu za nchi zilizowekwa, pia amesema ili mtu aweze kujenga katika Mkoa huo anatakiwa kuzingatia mambo matatu muhimu ambayo ni kuwa na Hati ya umiliki ya ardhi, mchoro ambao umeshibitishwa na Manispaa ya Morogoro pamoja na kibali cha ujenzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro ( MORUWASA) Mhandisi Tamim Katakweba amesema ujenzi wa tanki hilo lenye ujazo wa lita milioni mbili na limegharimu kiasi cha shilingi Milioni 486 litasaidia kupunguza kero ya maji katika maeneo ya kihonda, kihegea lenye wakazi zaidi ya Laki mbili na Ishirini.
Aidha, Mhandisi Katakweba ameongeza kuwa mahitaji ya maji katika Mkoa huo ni Lita milioni 71 kwa siku lakini kwa sasa maji yanayopatikana ni lita 36 kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 48 hivyo utekelezaji wa miradi hiyo katika Mkoa huo itapunguza kero ya upatikanaji wa maji.
Mkurugenzi huyo amesema Mradi wa uboreshaji wa bwawa la Mindu unatekelezwa kwa Bilioni 185 utahusisha uongezaji wa kina cha maji, ujenzi wa kituo cha kutibu maji katika eneo la Mafiga lenye ujazo wa lita milioni 54 pamoja na ujenzi wa matenki ya maji katika maeneo ya Lukobe.
sambamba na hilo Mkurugenzi huyo wa Moruwasa ameomba kupatiwa ardhi ili kuongeza ujenzi wa kituo cha kutibu maji katika eneo la kihonda Mizani pamoja na ujenzi wa Ofisi kubwa ya Moruwasa.
Ziara hiyo ya Mhe. Fatma Mwassa ilianzia katika kituo cha kupokelea maji cha Mambogo, alitembelea bwawa la Mindu pamoja na mradi wa ujenzi wa tanki la maji katika eneo la Kihegea.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.