Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi wa kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya Nanenane Kanda ya Mashariki, amewataka wakulima kuwa na uzalishaji wenye tija katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo ili kukidhi mahitaji ya nchi na kupanua wigo wa biashara ndani na nje ya nchi.
Mhe. Kindamba amesema hayo Agosti 8, 2023 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba (wa pili kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge, viongozi wengine katika picha hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge.
Mhe. Kindamba amesema kutokana na maonesho hayo anaamini kutakuwa na kilimo chenye tija kwa kujifunza teknolojia na mbinu za kisasa zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi kwani kwa kuongeza uzalishaji kupitia teknolojia mpya iliyotolewa Katika maadhimisho hayo itakuwa rahisi kupata masoko ya mazao hayo.
"... tutaweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji kwa ajili ya mahitajiya nchi yetu na ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi Sina shaka na wakulima, wafugaji na wavuvi na wadau wote ambao tumepata fursa ya kutembelea Maonesho haya tumejifunza teknolojia na mbinu mpya ambazo tukizitumia vizuri zitasaidia kuongeza uzalishaji..." amesema Mhe. Waziri Kindamba.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Waziri Kindamba akisalimiana na mkulima wa zao la vanila kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Aidha, Mhe. Kindamba amesisitiza kuwa teknolojia hizo za kilimo, ufugaji na uvuvi ziweze kuwafikia wakulima katika maeneo yao ili kuongeza ufanisi katika kazi na kutoa wito kwa sekta za umma na binafsi kushirikiana vyema na wakulima ili maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki kuendelea kuboreshwa kwa kuhimiza wadau kuleta teknolojia zitakazowapa elimu wakulima wa Kanda hiyo.
RC Kindamba akimkabidhi mkulima funguo ya trekta alilo nunua kutoka kampuni ya Agricom kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Hata hivyo, Mhe. Kindamba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku katika sekta ya kilimo na kupunguza bei za viwatilifu na mbolea, amesema Mhe. amefika hatua hiyo kwa kutambua umuhimu wa wakulima wenye hali ya chini ili kupata pembejeo hitajika hivyo kupata mazao ya kutosha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima Kwa niaba ya wanakamati wa Maonesho hayo Kanda ya Mashariki amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Bodi ya sukari Kwa kujitoa kufanikisha Maonesho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akipokea zawadi kutoka kwa viongozi wa Bodi ya sukari baada ya kutembelea banda hilo.
Mhe. Malima ameongeza kuwa wadau mbalimbali ambao walitakiwa kuongeza nguvu wajipange ili Maonesho yajayo yawe Bora zaidi na kutaka kuwa na vipando vya kudumu vya Maonesho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima katikati akiwa pamoja na Makatibu Tawala wa mikoa ya Morogoro na Tanga kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa, kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bi. Pili Mnyema.
Maonesho hayo yamehitimishwa rasmi Leo Agosti 8, 2023 hata hivyo kutokana na wananchi kuendelea kuhitaji Elimu mbalinbali Katika viwanja hivyo maonesho yataendeleo kwa siku mbili zaidi hadi Agosti 10 mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.