Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Emmanuel Mkongo kutoa mikopo ya 10% kwa kikundi cha Mama Lishe chenye idadi ya watu 32 walio jisajili katika Kituo cha Treni ya kisasa cha Manispaa ya Morogoro ili kupata mtaji wa kuendesha biashara zao.
Adam Malima ametoa agizo hilo Julai 12, Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya treni ya mwendo kasi - SGR hususan ya kituo cha treni hiyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni maandalizi ya treni ya SGR kuanza safari yake ya kutoa huduma kwa wananchi kutoka Dar es Salaam – Morogoro na Dodoma ifikapo Julai 25 mwaka huu.
Mhe. Adam Malima amesema reli hiyo ya kiwango cha kisasa itasaidia kukuza uchumi wa Mkoa huo na nchi kwa ujumla, hivyo wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kufanya shughuli za kiuchumi zikiwemo biashara, utalii na kilimo kwa maslahi mapana ya jamii na taifa.
Akifafanua zaidi kuhusu agizo la mikopo kwa akinamama hao amewataka kila mmoja kuweka bajeti ya kiasi anachotaka kukopa na wakishapata jumla ya kiasi chote waende kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro wakubaliane ili waweze kukopeshwa.
"... kaeni mkubaliane muunde kikundi kimoja mkienda Halmashauri mtaandikishwa mkikubaliana nendeni mkachukue mitaji ya 10% mboreshe biashara zenu..." amesema Mhe. Malima
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amewashauri wananchi hususan Mama lishe wanapochukua fedha za mkopo kutoka Halmashauri husika wajikite kuzalisha na kuwa waaminifu kurudisha fedha hizo ili kupewa watu wengine wenye uhitaji.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima ametoa siku 14 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kujenga vituo vya Maafisa usafirishaji wakiwemo Boda boda 250, madereva teksi 50 na waendesha pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama Bajaji 150 pamoja na kujenga eneo la Mama lishe ambao idadi yao ni 32 ili kuwa na maeneo maalum ya kufanyia kazi.
Kwa upande wake, Bi. Jamila Mbarouk, Mkuu wa Kitengo cha habari cha Shirika la reli Tanzania (TRC) amesema maafisa hao na Mama lishe hao wamesajiliwa na kutambuliwa rasmi na TRC wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo kwa lengo la kuwasafirisha abiria na kutoa huduma ya chakula abiria watakaposhuka kituoni hapo na kujipatia kipato.
Naye, Mwenyekiti wa kikundi cha Mama lishe Bi. Happiness Samuel Chilingo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ujio wake huku akitoa ombi la kupewa sehemu ya kufanyia biashara yao ya chakula.
Kwa upande wao Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wakiwakilishwa na Bw. Emanuel Jacob wamemuomba Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Kighoma Malima kutengenezewa barabara, sehemu ya kupaki pikipiki na kujengewa choo maombi ambayo yote ni ya muhimu, ameyapokea na kuwaahidi kuyafanyia kazi.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.