Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ameiagiza Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (MORUWASA) na Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha miradi ya maji inayotekelezwa ili kutatua kero ya maji kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa na Mkoa huo.
Mhe. Adam Malima ametoa agizo hilo Januari 8, 2025, wakati wa kikao cha 42 cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Magadu uliopo Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema suala la maji haliwezi kuvumilika hivyo hadi kufikia Januari 30 Mwaka huu Mamlaka hizo zimetakiwa kuandaa majibu ya namna ya kutatua kero hiyo ya maji.
… hadi tarehe 30 tunataka mje na majibu ya upatikanaji wa maji…” amesisitiza Mhe.Malima
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa huyo, amekemea tatizo la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto unaotokea Mkoani humo na kutaka zitafutwe njia za kutatua tatizo hilo kwani amesema jamii inapaswa kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwemo unyanyasaji wa wanawake, ubakaji, vitisho na ulawiti na matukio mengine yanayofanana na hayo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka viongozi wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji au Mitaa kushirikiana kuandaa mipango madhubuti ya kuondoa ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli, amesema uwepo wa sheria nyepesi ndio sababu kubwa inayosababisha matukio ya ukatili Mkoani humo kuendelea kwa kasi.
Kwa sababu hiyo, Wajumbe wa kikao hicho kwa kauli moja wamekubaliana kupeleka kwenye mihimili ya kutunga sheria mapendekezo ya kubadilisha au kukaza sheria zilizopo ili wale wanaobainika kujihusisha kufanya vitendo vya ukatili waadhibiwe kwa sheria hizo mpya.
Akiwasilisha mada hiyo Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Morogoro, ASP. Dkt. Mwanaidi Lwena, amesema kuwa ukatili wa kijinsia huathiri afya ya mwili na akili, na wakati mwingine kusababisha vifo, hivyo ameshauri kuwepo kwa mfumo unaoharakisha huduma za matibabu, ushauri nasaha, na ufuatiliaji wa kesi za waathirika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga, watendaji kutekeleza kazi zao kwa weledi ili kukamilisha maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hususan katika kusimamia miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.
Akiwasilisha mada ya Sehemu ya Mipango na Uratibu Bw. Eric Olomi amesema kwa Mwaka wa fedha wa 2024/2025 Mkoa wa Morogoro umeidhinishiwa kutumia shilingi Bil. 4.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni shilingi Bil. 3.4 na fedha za nje ni shilingi Bil. 1.4 ambapo zitatumika katika ujenzi wa miradi ya maendeleo na kukamilika kwa wakati.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.