Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani humo pamoja na vyombo vingine vya usalama kuchunguza maendeleo ya mradi wa skimu ya umwagiliaji wa Mgongola iliyopo Wilayani Mvomero ili kujua ukweli wa sababu zinazopelekea mradi huo kutokamilika.
Mhe. Adam Malima ametoa agizo hilo leo Machi 3, 2025 wakati wa kikao cha kujadili hali ya mradi huo wa umwàgiliaji, kikao ambacho kimehusisha uongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wizara ya Kilimo pamoja na Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni M/S BADR EAST AFRICA ENTERPRISES LIMITED kikiwa na lengo la kutatua changamoto za mradi huo.
Amesema, TAKUKURU inapaswa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini changamoto ya kutokamilisha mradi huo iko upande gani kati ya wataalam wa serikali na mkandarasi anayetekekeza mradi ili kunusuru fedha za Serikali kutotumika ipasavyo badala yake mradi huo ukamilike na kuwaletea faida wananchi kama Serikali ilivyokusudia.
"...TAKUKURU, uhamiaji na vyombo vingine vya usalama nendani na hawa mabwana mkafanye uchunguzi halafu mje na majibu ili tutatue hili jambo..." ameagiza Mhe. Malima.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) aliyeshiriki kikao hicho mwanzo hadi mwisho sambamba na maagizo hayo ya Mkuu wa Mkoa amesema Serikali haiwezi kufurahishwa na maumivu na kodi ya watanzania kwa sababu ya mtu mmoja na kuathiri watanzania walio wengi.
Aidha, Mhe. Silinde amesema Serikali ina nia njema na wananchi wake hivyo mkandarasi anapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wote wa serikali ili kufanikisha mradi huo kwani amesema kufanya kazi kinyume na mkataba kunaongeza gharama za mradi na kuathiri manufaa ya mradi kwa wananchi na muda wa mradi kukamilika.
Mradi huo ambao kwa mujibu wa mkataba hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi Bilioni 5.6, unajengwa na mkandarasi M/S BADR EAST AFRICA ENTERPRISES LIMITED tangu mwaka 2022 bila kukamilika na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Mvomero ambao ndio wanufaika wa mradi huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.