Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameuagiza uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi Mkoani humo kutoa Elimu kwa wakulima wa miwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kuwa na Mali ghafi ya kutosha kulisha Kiwanda hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (wa tatu kushoto) akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali wakitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda kipya cha sukari cha Mkulazi wakijionea maendeleo ya ujenzi wake.
Mhe. Adam Malima ametoa agizo hilo Julai 23 mwaka huu alipofanya ziara ya siku moja katika kiwanda kipya cha Sukari cha Mkulazi kilichopo Mbigiri Wilayani Kilosa ambacho kinamilikiwa na Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) pamoja na Jeshi la Magereza.
Muonekano wa kiwanda kipya cha sukari cha Mkulazi kilichopo Mbigiri Wilayani Kilosa ambacho kitazalisha tani 50,000 kwa mwaka.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Kiwanda hicho ambacho kitazalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka kitapunguza uagizaji wa shehena za sukari kutoka nje ya nchi hivyo kitachangia upatikanaji wa ajira kwa watanzania.
Aidha, ameuagiza uongozi wa kiwanda hicho kuwaandaa wakulima ambao watazalisha miwa itakayo kidhi mahitaji ya kiwanda hicho.
“...sasa hawa wakulima wadogo huwa wanaandaliwa na ndivyo tulivyokubaliana sasa hivi na Bodi na watu wengine kuwa watengeneze mpango wa kuwaandaa wakulima ili waweze kuendana na mahitahi ya kiwanda...”. Amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemtaka Mkandarasi anaye tekeleza mradi huo kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kianze uzalishaji wake.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuanzisha Kiwanda cha sukari cha Mkulazi ambacho kitazalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka hapa nchini.
Nae, Bw. Filbert Mpozi Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 Serikali haiagizi sukari kutoka nje, hivyo kiwanda hicho kipya kitatimiza lengo lake kutoagiza Sukari nje ya nchi.
Aidha, ameongeza kuwa kiwanda hicho kitaifanya Serikali kutotumia fedha nyingi za kigeni kuagiza sukari nje ya nchi lakini pia kiwanda hicho kitaongeza ajira kwa watanzania.
Hata hivyo, Bw. Filbert ameipongeza Serikali kupitia NSSF kwa uwekezaji huo ambao utaisaidia nchi kujitegemea kwenye bidhaa ya sukari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mkulazi Holding Company Dkt. Hildelitha Msita kwa niaba ya wajumbe wa Bodi hiyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara yake na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo aliyoyatoa ikiwemo kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.