Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemuahidi Bw. Seleman Msindi maarufu kama “Afande Sele” ambaye ni Balozi wa Mazingira hapa nchini kumpa kila ushirikiano katika kufanikisha azma yake ya kufikisha elimu ya mazingira kwa jamii.
Mhe. Malima ameyasema hayo Disemba 20 mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kuzungumza na Afande Sele ofisini kwake kuhusu utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji hapa nchini.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, wajibu wa kila mmoja ni kutambua umuhim wa utunzaji wa mazingira na elimu hiyo ya mazingira ni muhim iwafikie watu wengine huku akimuhakikishia Balozi huyo kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza jambo hilo la kitaifa.
“...na mimi nataka nimuhakikishie tu kwamba Serikali ya Mkoa wa Morogoro itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba inampa ushirikiano katika kutekeleza hili...” amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Malima amesema Ofisi yake itahamasisha wadau wa wengine wa mazingira Mkoani humo ili waweze kushirikiana na Balozi huyo katika kufikisha elimu ya utunzaji wa mazingira kwa jamii, lengo likiwa ni kutimiza azma yake.
Sambamba hilo Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira hapa nchini.
Kwa upande wake Afande Sele ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Afande Sele Foundation (ASEFO) ambaye pia ni Balozi wa Mazingira, amesema lengo la kukutana na Mkuu huyo wa Mkoa ni kuomba uwezeshaji kutoka Ofisi yake na wadau wengine wa mazingira ili aweze kufikisha elimu ya utunzaji wa mazingira kwa jamii.
Afande Sele, ametoa wito kwa jamii kutimiza wajibu wao kwa vitendo katika utunzaji wa mazingira kutokana na kwamba athari za mazingira zinamgusa mtu yeyote hapa Duniani.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.