Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaeleza wadau wa mpira wa miguu na umma wa watanzania kwa ujumla kuwa hali ya uwanja wa mpira wa miguu wa Jamhuri Mkoani humo uko vizuri na marekebisho ya kuelekea mechi ya timu ya Yanga Sports Club dhidi ya KMC unaotarajiwa kuchezewa februari 17, 2024 katika uwanja huo yako vizuri.
Mhe. Malima amesema hayo Februari 10, 2024 baada ya kufanya ziara mahususi ya kuutembelea uwanja huo na kukagua maeneo ya ukarabati yanayoendelea kufanywa katika uwanja huo wa Jamhuri uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kufanyika marekebisho ya sehemu ya kuchezea (pitch) limeridhishwa na ukarabati huo, huku jitihada za kukarabati vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji zikiendelea na kuhakikisha miundombinu mingine yote iliyobaki ukarabati wake unakamilika kwa wakati.
“….. Siku hizi mpira wa miguu unahusishwa na shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo sisi tunaiangalia hii Morogoro kama ni mji wa mpira na kwa maana hiyo starehe hiyo ya kuhakikisha mpira unachezwa vizuri morogoro lazima ianzie hapa Jamhuri Stadium….” amesema Adam Malima.
Mhe. Malima amesema kuanzia mwezi Novemba, 2023 wamekuwa na mikakati ya kuuboresha uwanja huo ikiwemo kurudisha majani, kurudisha kijani, kuondoa sehemu za vipara pamoja na kusawazisha sehemu ya mashimo ya uwanja huo na kurudisha hali ya upatikanaji wa maji ya kumwagilia uwanja huo.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima ameishukuru timu ya mpira wa miguu ya KMC kwa kuleta mechi hiyo uwanja wa Jamhuri - Mororgoro kama uwanja wao wa nyumbani huku akibainisha kwamba mechi hizo zinasaidia kuingiza mapato kwa Halmashauri husika na kwamba halmashuri ya Manispaa ya Morogoro itakusanya mapato kutokana na ukubwa wa mechi hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa uwanja wa CCM Jamhuri Morogoro, John Simkoko amesema kuna maelekezo walipewa na TFF yakiwemo marekebisho ya sehemu ya kuchezea, kukarabati vyumba vya kubalishia nguo wachezaji pamoja na kurekebisha vyoo vya uwanja huo.
Hivyo, amemshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Ali Malima pamoja na wadau wengine wa kabumbu mkoani humo kwa kuhakikisha ukarabati wa uwanja huo unakamilika kwa wakati na kuweza kufikia ubora unaotakiwa na shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania - TFF.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.