Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima abaini uwepo wa makundi makubwa ya mifugo katika Pori la Akiba Kilombero na kutaka kujipanga zaidi ili kuwaondoa mifugo waliomo kwa lengo la kuhifadhi pori hilo ambalo ni moja ya chanzo kikubwa cha maji yanayo kwenda kufua umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo ya uwepo wa makundi makubwa ya mifugo ndani ya pori hilo Januari 20, 2024 mara baada ya kurejea kukagua pori hilo kwa njia ya ndege na kugundua uharibifu mkubwa unaoendelea kufanyika humo hususan kilimo na Ufugaji.
Kwa sababu hiyo, Pamoja na kuendelea na juhudi za kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu umuhim wa pori hilo, Mhe. Malima amesema ni muhim kuwa na muda wa kujipanga zaidi katika kuliendea zoezi nzima la kuondoa makundi makubwa ya mifugo yaliyomo ndani ya Pori hilo la akiba.
“hayo maboma ya ng’ombe sio moja mawili matatu, hilo bonde lina maboma ya ng’ombe karibu mia tano…” amebainisha Mhe. Adam Malima.
Katika hatua nyingine, Kiongozi huyo wa Mkoa ameagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania - TAWA kuimarisha kitengo cha wanamaji kilichopo ndani ya Taasisi yao ili kiweze kupambana na makambi makubwa ya wavuvi yaliyopo katika Pori hilo ambayo hayafikiki kirahisi kwa miguu.
Sambamba na maagizo hayo, Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Malima ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania – TAWA kwa kazi kubwa wanayofanya katika mazingira magumu ya uhifadhi wa pori hilo la Akiba.
Baada ya ziara yake ya angani kutembelea bonde akiba Kilombero, siku hiyo hiyo, Mkuu wa Mkoa Adam Malima akafanya mikutano ya hadhara katika kijiji cha Lupilo na Kitongoji cha Ipela/Mbenja Wilayani Ulanga na kusisitiza umuhim wa utunzaji wa Pori la akiba Kilombero kwa maslahi mapana ya Taifa hususan upatikanaji wa umeme.
Kwa upande wao wananchi wa maeneo hayo walimuomba Mkuu wa Mkoa kuendelea kwa muda na kilimo katika maeneo waliyopo hadi mazao yao yatakapokomaa na kuvunwa ndipo waachie maeneo hayo ambayo ki msingi wengi wanakiri kuingia kimakosa maeneo hayo ombi ambalo lilikubaliwa na Mkuu wa Mkoa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.