Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema usimamizi mbovu wa mikopo ya asilimia 10 ya Wanawake, Vijana na wenye ulemavu umepelekea Serikali kusitisha utoaji wa Mikopo hiyo kwenye Halmashauri hapa nchini.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Novemba 2 mwaka huu kwenye mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali na waandishi wa Habari uliolenga kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita Mkoani Morogoro, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha sababu zilizopelekea Serikali kusitisha utoaji wa mikopo hiyo kuwa ni uwepo wa baadhi ya vikundi hewa, ucheleweshaji wa malipo kutoka kwa vikundi vilivyokopa mikopo hiyo, lakini amesema kuwa pale ambapo kuna usimamizi mzuri wa mikopo hiyo wananchi wamenufaika na mikopo hiyo.
“...tukumbushane tu kwamba ile mikopo ya asilimia 10 haikuzuiliwa kwa sababu ya sera yenyewe ya mikopo, mikopo ile ilizuiliwa kwa sababu ya usimamizi mbaya wa ile mikopo...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amesema MkoaO umepanga kuomba vibali vya utoaji mikopo kwa vikundi vyenye malengo maalum hususan kuongeza tija ya uzalishaji hiyo pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo hiyo hususan usaili wa vikundi vitakavyo omba mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika maendeleo ya Mkoa huo ambapo hakuna Wilaya ambayo imeachwa nyuma kimaendeleo hususan ya kiuchumi, kijamii, kisiasa. Hata hivyo amesema Mkoa unajivunia uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Dkt. Samia katika sekta ya Umma na binafsi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.