Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ametaka uwepo ushirikiano wa kutosha baina ya mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali kwa kuwa na misingi ya kuaminiana kwa kila pande ili kulinda maslahi ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Malima ametoa rai hiyo Disemba 18, Mwaka huu wakati wa kikao na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) Mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkoa huo kikiwa na lengo la kuweka mikakati na maazimio ya namna ya kufanya kazi pamoja.
“... Leo tumejenga misingi ya kuaminiana na kuambiana lakini pia kutambua kwamba hakuna uhuru usio na mipaka wao ni mashirika yasiyo ya kiserikali lakini miongozo ipo ya kufuata...” amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema mashirika hayo yana uhuru wa kufanya kazi lakini yanapaswa kushirikiana na serikali ili kuendelea kuondoa kasoro ndogo ndogo zilizopo na kuyataka kufuata taratibu, kanuni na sheria za kujisajili na namna ya kuendesha kazi zao kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika yasiyo ya kiserikali Taifa Bi. Mwantumu Mahiza amezitaka NGOs Mkoani humo kufanya kazi zao kwa uwazi, ukweli na kujituma zaidi kwa kujua kuwa wanafanya kazi pamoja na serikali katika maeneo yao na kwa kushirikiana na madiwani, wenyeviti wa vitongoji na vijiji.
Awali, Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Morogoro Bi. Adelfina Pacho amesema kikao hicho kimelenga kulenga kujenga ushirikiano mzuri baina ya NGOs na serikali ndani ya Mkoa huo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye, Mwakilishi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Morogoro Bw. Otanamus Nicholas ameyashukuru mashirika hayo kushiriki kikao hicho ambapo amesema kimeweka wazi utekelezaji wa kila shirika na kunuia kufanya kazi na Serikari inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwaletea tija wananchi wake.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.